MBUNGE wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde amewataka wajasiriamali waliopo katika makundi maalum jijini Dodoma kuchangamkia fursa za zabuni mbalimbali zinazotangazwa na serikali na kwa kuwa sheria ya manunuzi ya umma imeweka bayana fursa hiyo.
Mavunde ameyasema hayo mjini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya uchakataji na usindikaji wa bidhaa chini ya mwavuli wa ‘Wanawake na Uchumi wa Viwanda’ (WAUVI).
Amesema mafunzo wanayoyapata yatachochea uongezaji wa thamani wa bidhaa zao na upatikanaji wa soko la uhakika.
“Tunao wajibu wa kuhakikisha mnapata mafunzo stahiki na kupata mitaji ya uhakika itakayowasaidia kuzifikia fursa mbalimbali hasa za serikalini.”Amesema Mavunde
Amesema, kifungu cha 64(2)(c) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma 2011 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 ukisoma sambamba na Kanuni Na. 30C ya Tangazo la Serikali Na. 446/2013 linazitaka Taasisi zote nunuzi za serikali kutenga asilimia 30 ya manunuzi yake kwa mwaka kwa ajili ya wakina mama,vijana na watu wenye ulemavu hivyo ni lazima kuhakikisha fursa hazipiti na serikali inakuwa sehemu ya manunuzi hayo ya umma.
“Kwa nafasi yangu nitaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba wajasiriamali Jijini Dodoma mnanyanyuka kiuchumi na kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.”Alisema Mavunde
Naye Mwenyekiti wa WAUVI Rehema Mbeleke amesema mafunzo hayo yanayoratibiwa na SIDO yana lengo la kumjengea uwezo mjasiriamali wa Dodoma kulifikia soko kwa urahisi na akachukua nafasi hiyo kumshukuru Mbunge Mavunde kwa kuwachangia Tsh 1,000,000 ya vifaa vya kufundishia pamoja na na kuwanunulia printer ya ofisi kwa ajili ya uratibu wa kazi za kila siku za WAUVI.
Post A Comment: