Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge amesema Tanzania imeendelea kushirikiana na Shirika la Afya Duniani na wadau mbalimbali katika kuhakikisha inatekeleza kanuni za Afya za kimatiafa, Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko na utekelezaji wa mkakati wa Afya Moja.
Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi cha kuongeza Uelewa juu ya kanuni za Afya za Kimataifa, Afya Moja na Muongozo wa ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko (IDSR) kilichofanyika mapema Aprili 3, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Dodoma hoteli.
Meja Jenerali Charles Mbuge amesema lengo la kikao kazi hiki ni kuhakiksha hatua stahiki zinachukuliwa kwa wakati iwapo kuna matukio, dharura au majanga yenye athari za kiafya yanapojitokeza.
“Magonjwa tunayokabiliana nayo hayana mipaka na hivyo inatupasa kila mmoja katika nafasi yake kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha usalama kwa watu wetu na kufanyia kazi taarifa zozote zikiwemo za tetesi (rumours) tunazozipokea kupita vyanzo mbalimbali vya habari hata kama magonjwa/matukio haya yapo nchi jirani”. Alisema Meja Jenerali
Aidha Meja Jenerali amesema mada zitakazo zungumziwa katika kikao ni pamoja na mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya milipuko ambapo Mfumo huo unatumika kukukusanya taarifa ambazo zinazalishwa na vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo mpaka sasa vinafikia 7789 vikiwa na watoa taarifa waliosajiliwa zaidi ya 12,000.
“Ndugu washiriki Mfumo huu unapokea taarifa za matukio yenye athari kiafya kutoka katika vyanzo visivyo rasmi ikijumuisha kutoka kwenye jamii, vyombo vya habari na vyanzo vingine vya habari nia ikiwa kupata taarifa mapema kabla ya kuleta madhara makubwa kwa jamii pia utawapa uelewa wa kushirikiana katika kudhibiti magonjwa ya milipuko kwa kutoa taarifa mapema na kuchukua hatua nyingine stahiki”.alisema Meja Jenerali Mbuge
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kitengo cha Afya Moja Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Salum Manyatta amesema mafunzo haya hasa kwa wajumbe kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama yatarahisisha kusaidia utoaji na upatikanaji wa taarifa pindi Magonjwa ya Mlipuko yanapotokea.
“Kikao hiki pia kimehusisha vyombo vya ulinzi na usalama huwa tunatoa mafunzo kwa kada na watumishi mbalimbali maana tunavituo vingi vinavyo toa taarifa hivyo mafunzo haya yatasaidia kuhakikisha tunadhibiti magonjwa lakini pia utoaji taarifa wenye mpangilio”.alisema Dkt. Salum
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
Post A Comment: