Na John Walter-Babati

Viongozi wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wilaya ya Babati kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Manyara  wameendelea kutoa elimu kwa wanafunzi katika shule mbalimbali juu Ukatili wa Kijinsia.

Akizungumza na wanafunzi na walimu katika shule ya msingi Kiru six na Shule ya Sekondari Kiru six, Mkuu wa Dawati la jinsia Mkoa, Willnes Kimario amewataka wanafunzi  kutoa taarifa wanapofanyiwa ukatili au wanapoona ukatili unafanyika katika maeneo yao.

Amesema ili kukomesha vitendo vya ukatili na ukeketaji katika mkoa wa Manyara ni lazima kila mmoja ashiriki katika vita hivyo kwa kuwafichua wahusika ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua.

Willnes amesema vitendo vya ukatili wa kijnsia kwa watoto na wanawake katika mkoa wa Mnayara vinaendelea kushamiri kwa kuwa wahusika hawatoi ushirikiano mahakamani na kumaliza kesi nyumbani.

Mwenyekiti wa Smaujata wilaya ya Babati Philipo Sanka amesema wanaendelea na maandalizi ya kambi maalum ya kitaifa kwa ajili ya elimu ya masuala ya ukatili katika jamii ambayo itafanyika katika kata ya Kiru six mwezi wa sita.

SMAUJATA Babati wanatembea na kauli mbiu isemayo “Usalama wetu kwanza”

Katibu msaidizi SMAUJATA Mkoa wa Manyara Rest George Chuhila amewataka wanafunzi hao wasikubali kurubuniwa na wazazi au walezi kuacha masomo na kuolewa kwa kuwa umri wa kuolewa ni kuanzia miaka 18 baada ya kumaliza kusoma shule ya Msingi, Sekondari na chuo.

Aidha afisa Maendeleo ya jamii Babati Agatha Patrice, amewataka Wanafunzi wawe mabalozi wazuri katika familia zao kupinga vitendo vya ukeketaji na kuwataka vijana wa kiume  kutoa taarifa wanaposikia tetesi za kufanyika kwa ukeketaji.

Mkaguzi wa Polisi kata ya Kiru Six Ali Ibrahim amewataka wanafunzi waridhike na hali walizonazo wazazi wao na kuacha tabia ya kutamani vitu vilivyo nje ya uwezo wao kwani ndo chanzo cha kufanyiwa ukatili.

Kwa siku moja pekee April 13, 2023, SMAUJATA wilaya ya Babati na Dawati la jinsia Polisi mkoa wa Manyara walitoa elimu kwa wanafunzi 1,500 wa shule ya msingi kiru six na wa sekondari ya kiru six Zaidi ya 600.


 

 

Share To:

Post A Comment: