Mkaguzi wa Polisi Amina Abdallah wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Singida akizungumza katika Siku ya Mtoto wa Kike iliyoandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

...........................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

WANAUME wametakiwa kujichunguza na kujitathimini kutokana na kudaiwa kuwa ndio chanzo cha mambo mbalimbali ya ukatili wa kijinsia ukiwemo ubakaji na kutelekeza familia.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Mkaguzi wa Polisi Amina Abdallah wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Singida wakati akizungumza katika Siku ya Mtoto wa Kike iliyoandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida na kuhudhuriwa na wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma na Chuo cha Ufundi Stadi VETA ambapo mada mbalimbali zilitolewa.

"Hawa wanaume wanapaswa kujichunguza na kujitathimini kutokana na maeneo mengi kuhusika nayo, wanao tia mimba ni wao, wanaobaka ni wao, wanao telekeza familia ni wao, wanaofanya vitendo vya ushoga ni wao yaani kila eneo la ukatili hawakosekani kwa kweli wanapaswa watuambie wanashida gani" alisema Abdallah.

Alisema wanaume ndio chanzo cha kuwepo kwa watoto wa mitaani kwani wengi wao wamekuwa wakikimbia majukumu ya kulea familia baada ya kuwazalisha wanawake na kisha kuwakimbia jambo ambalo limekuwa likiwafanya wakina mama kujiingiza kwenye vitendo vya ukahaba ili wapate fedha za kujikimu na watoto wao.

Mkaguzi Abdallah aliongeza kuwa watoto hao kuwa katika mazingira magumu kufuatiwa mama zao kutelekezwa na wanaume waliowapa mimba kumesababisha kukosa uangalizi mzuri wa malezi na matokeo yake kujikuta wakiwa katika hatari ya kubakwa na kulawitiwa.

Mkaguzi huyo alikwenda mbali zaidi na kusema wanaume wanapaswa kuogopwa kutokana na kuwa vinara wa mambo yoteya ukatili wa kijinsia na kuwataka wanawake wanapoachana na wenza wao wasikubali kuwaacha watoto kwa wanaume zao wawe wa kiume au wa kike.

Alisema kumekuwa na kesi nyingi za wanaume kudaiwa kuwabaka na kuwalawiti watoto wao ambapo alitolea mfano moja ya tukio la mwanaume mmoja aliyeachana na mke wake kumuingilia binti yake wa miaka 11 na kumlawiti hadi kufikia hatua ya kutoa haja kubwa kila wakati ambapo kwa msaada wa jeshi la polisi alipelekwa Hospitali ya Manispaa ya Singida kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Afande Abdallah aliwahimiza wanafunzi hao kuzingatia masomo na kuacha kujiingiza katika masuala ya mahusiano ya kimapenzi kwa ajili ya kushawishiwa kwa fedha na vitu vingine.

Alisema kujihusisha na mapenzi kunawaweka katika mazingira ya kupata mimba na kueleza kati ya miezi miwili iliyopita maiti sita za vichanga wanao kadiriwa kuwa wa miezi kuanzia mitatu hadi nane ziliokotwa na jeshi la polisi katika maeneo mbalimbali karibu na chuo hicho na maeneo ya Sabasaba.

Akizungumzia masuala ya mapenzi ya jinsia moja aliwata wanafunzi hao kuacha kununua vitu mbalimbali ambavyo vinatangaza mambo hayo kama kununua nguo, vifunika simu, nguo na vitu vingine vinavyofanana na rangi zinazotumika kuhamasisha ushoga na usagaji.

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Sifa Mwanjala akitoa mada iliyohusu elimu ya mtoto wa kike katika kupambana na rushwa akiwa chuoni alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya rushwa ya ngono na akawataka wanafunzi hao kuchukua tahadhari nayo.

Alisema mtu yeyote anapokuwa anaikataa rushwa ya ngono anakuwa ameilinda heshima yake na utu wake ambapo aliwahimiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujiamini na kuacha tabia ya kutegemea kubebwa na watu jambo ambalo wanaweza kujikuta wakiingia katika rushwa ya ngono.

Daktari Salum Mgeleka kutoka  Shirika la Elizabeth Glaser Pediatic Aids Foundation (AGPAF) kupitia mradi wa USAID Afya Yangu Mkoa wa Singida, akitoa mada kuhusu Elimu ya Afya ya Uzazi na Magonjwa ya Zinaa wanayoyakabili watoto wa kike alisema katika Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka jana, idadi ya wanaume na wanawake Mkoa wa Singida ilikuwa ni sawa kwa asilimia 50 kwa 50.

Alisema katika maambukizi ya virusi vya Ukimwi imekuwa ni tofauti kwani wanawake wamekuwa ni asilimia 82 huku wanaume wakiwa na asilimia 18 tu na kuwa waathirika zaidi ni wenye umri kuanzia miaka 10, 20 hadi 30 ambao wengi wao ni kundi la vijana.

Alisema baada ya kuwa hoji wanafunzi hao sababu ya wanawake kuwa na asilimia kubwa ya maambukizi alisema walidai kuwa moja ya sababu ni ajira nyingi zimekuwa zikitolewa kwa wanaume kuliko wao, sababu ya maumbile yao na mambo mengine.

Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Singida, Christoweru Barnabas akitoa Elimu ya Afya ya Uzazi na Magonjwa ya Zinaa aliwataka wanafunzi hao kutojiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi na kufanya ngono zembe na kuwa kama watashindwa kujizuia watumie kinga.

Alisema wakijiingiza katika mahusiano hayo kwa tamaa ya fedha na vitu vingine watakuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama, gono, kaswende, samaki na mengine na kuwa iwapo watabainika kupata maabukizi hayo ni vizuri kwenda vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu na sio vichochoroni.

Aidha alitoa tahadhari kwa wanafunzi hao kuacha tabia ya kutumia dawa za kuzuia kupata mimba bila ya kufuata taratibu au ushauri wa daktari kwani  zinaweza kuwasababishia ugumba na kuja kujuta baadae.

Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi  wa Jamii (SMAUJATA) Mkoa wa Singida, Happy Francis ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wezesha Mwanamke mkoani hapa akizungumza na wanafunzi hao alisema kumekuwa na ukatili wa kijinsia ambao umewaathiri watu wengi wakiwemo wanafunzi.

Alitaja baadhi ya aina ya ukatili huo kuwa ni wa kiuchumi, kingono, kisaikolojia, kimwili na kuwa kila mmoja anapaswa kuchukua hatua za kupambana nao kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali likiwepo jeshi la polisi.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Manispaa ya Singida, Stara Beka aliwataka wanafunzi hao kuchangamikia mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri za wilaya kwa vijana, walemavu na wanawake kwa ajii ya kukopa ili waweze kuanzisha biashara ndogondogo zitakazo wasaidia kiuchumi badala ya kukaa bure.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la  Empower Society Transform Lives (ESTL), Joshua Ntandu akizungumza katika siku hiyo alisema ukatili wa kijinsia wa aina zote haukubaliki na akasema iwapo kutakuwa na ukatili katika eneo lolote shirika hilo lina namba ya siri ambayo inatumika kutoa taarifa kwa kutumia ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi kwa namba 0710567003 ujumbe ambao utatumwa Jeshi la Polisi, Ustawi wa Jamii na Vituo vya Afya.

Akitoa mada kuhusu siasa na maendeleo ya Jamii katika kumuandaa mtoto wa kike, Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Violet Soka aliwahimiza wanafunzi hao kushiriki katika siasa kwani inawaandaa kuwa viongozi akiwatolea mfano Rais Samia Suluhu Hassan,Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na wengine wote ambao waliingia kwenye siasa na leo wameshika madaraka makubwa.

Alisema pamoja na kuwa katika siasa jambo kubwa linalohitajika ni kufanya siasa safi za kuwaletea maendeleo wananchi katika nyanja mbalimbali kama anavyofanya Mwanamke wa nguvu Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwangalizi wa Wanafunzi wa TIA, Kampasi ya Singida, Ambwene Kajula, alisema siku hiyo ya mtoto wa kike imekuwa ya mafanikio makubwa kwani wameweza kutoa mafunzo mbalimbali ya afya ya uzazi, kukua kiuchumi na kuwaonesha jinsi  ulimwengu wa kidigitali ulivyo na nguvu ya kujiletea maendeleo pamoja na namna ya kujikinga na ukatili wa kijinsia na utoaji wa taarifa ya matukio hayo. 

Katika siku hiyo wanafunzi wa Taasisi hiyo walipata fursa ya kuonesha vipaji vyao mbalimbali kama vya muziki, ulimbwende na mitindo.


Mwalimu Suzana Mkoko wa TIA, Kampasi ya Singida  akizungumza kwa niaba ya Mkurugnzi wa Chuo hicho katika siku hiyo.

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Sifa Mwanjala akitoa mada iliyohusu elimu ya mtoto wa kike katika kupambana na rushwa akiwa chuoni.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la  Empower Society Transform Lives (ESTL), Joshua Ntandu akizungumza katika siku hiyo.
Daktari Salum Mgeleka kutoka Shirika la Elizabeth Glaser Pediatic Aids Foundation (AGPAF) kupitia mradi wa USAID Afya Yangu Mkoa wa Singida, akitoa mada kuhusu Elimu ya Afya ya Uzazi na Magonjwa ya Zinaa wanayoyakabili watoto wa kike.
Mwangalizi wa Wanafunzi wa TIA, Kampasi ya Singida, Ambwene Kajula akizungumzia siku hiyo.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa,
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Makamu wa Eais wa TIA, Witness Boniphace akizungumza katika sikuhiyo.
Wanafunzi wa VETA wakiwa kwenye siku hiyo.
Viogozi wakiwa meza kuu.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Violet Soka akizungumzia kuhusu namna ya kuwaanda viongozi.
Wanafunzi wa kifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa.
Taswira ya siku hiyo
Dk. Roza Majemgo akizungumza kwenye siku hiyo
Wanafunzi wakiwakwenye siku hiyo
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Singida, Christoweru Barnabas akitoa Elimu ya Afya ya Uzazi na Magonjwa ya Zinaa.

Kaimu Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi  wa Jamii (SMAUJATA) Mkoa wa Singida, Happy Francis ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wezesha Mwanamke mkoani hapa akizungumza na wanafunzi hao
Afisa Mauzo wa Benki ya CRDB Mkoa wa Singida, Clara Venance akielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na benki hiyo.
 Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Manispaa ya Singida, Stara Beka akizungumzia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri za wilaya nchini.
Msanii Laula wa TIA, akionesha kipaji cha kuimba.
Mwanamuziki Aziza Ramadhani (Maarufu Kenan) ambaye ni Mwanafunzi wa TIA, akionesha kipaji cha kuimba.
Miss TIA,Kampasi ya Singida, Nyamizi Edward akifanya vitu vyake kwenye siku hiyo.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: