Na John Walter-Kondoa
Wanakijiji wa Mitati kata ya Kikore wilayani Kondoa mkoani Dodoma wameandamana wakidai mwenyekiti wa kijiji amehamisha mradi wa maji kutoka kwenye eneo lao la mitati katai kwenda kitongoji cha Kiroroma.
Wananchi hao wamesema wanashindwa kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo kwa kuwa wanatumia muda mwingi kufuata maji umbali mrefu kwenye madimbwi ambayo sio safi na salama.
Wamesema walipoona uchimbaji wa visima unafanyika walipata matumaini ya kupata maji lakini ghafla mambo yakawa tofauti na walivyotarajia kwani tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi hawakuwahi kupata huduma ya maji safi na salama.
Mhandisi wa Maji kutoka wakala wa maji Vijijini (RUWASA) wilaya ya Kondoa Merinyo Saning’o amesema tuhuma kuwa viongozi wa kijiji wamehamisha mradi huo sio za kweli na kwamba kijiji cha Mitati na vitongoji vyake vyote vitapata maji kupitia mradi wa Innovation Africa unaofadhiliwa na Wafadhili kutoka Israel na Marekani.
Amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu.
Amesema walipima maeneo ambayo watapata maji ambapo walipochimba kisima mita 40 katika kitongoji cha Mitati kati palititia na kuanza kujifukia hali iyowalazimu kuondoa mitambo na kuhamishia pointi ya pili kitongoji cha Kiroroma.
Kutokana na kuwa mwenyekiti wa kijiji anatokea katika kitongoji hicho wananchi wakapata mashaka kwamba huenda mradi umehamishwa kwa ajili hiyo.
"Mradi huo haujahamishwa kutokana na sababu za kisiasa au kwa ajili ya mtu mmoja, ni mambo ya kitaalamu" alisema Mhandisi Merinyo
Ameongeza kuwa wafadhili hao hawataondoka katika kijiji cha Mitati hadi kumaliza changamoto ya maji inayowakabili kwa sasa.
Amesema RUWASA, wafadhili na wananchi walifanya kikao na kukubaliana kuhusu mradi huo wa kuchimba visima ambapo wananchi watalazimika kuchimba mitaro tu.
Diwani wa kata ya Kikore Ngware Salimu amesema yeye hana taarifa juu ya mradi huo.
Alipotafutwa kwa njia ya Simu mkuu wa wilaya ya Kondoa Hamisi Mkanachi alipokea na kuahidi kufuatilia juu ya suala hilo.
Post A Comment: