Eng Harryson Rwehumbiza afisa mazingira Kiwanda cha AtoZ akipokea maelekezo kutoka NEMC.
Na Jane Edward, Arusha
Kiwanda kinachozalisha nguo,net pamoja na bidhaa zingine za plastic cha AtoZ kilichopo Mkoani Arusha kimeagizwa kusitisha shughuli zote zinazozalisha maji taka kutokana na mfumo wa maji taka wa kiwanda hicho kushindwa kukidhi matakwa ya kimazingira kwa muda mrefu hali iliyopelekea wananchi kuathirika kiafya kutokana na maji hayo.
Hayo yamebainishwa na Mhandisi Ledemta Samweli mkurugenzi wa uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria Baraza la Mazingira Tanzania Makao Makuu wakati wa ziara maalum katika kiwanda hicho cha AtoZ.
Ziara hiyo imekuja mara baada ya Waziri wa Mazingira Dkt Suleimani Jafo alipotembelea kiwanda hicho hivi karibuni na kuagiza Taasisi ya NEMC kufuatilia malalamiko ya wananchi ambayo ofisi yake iliyapokea.
Amesema kuwa NEMC imekuwa ikifuatilia malalamiko ya wananchi kwa wa kata ya Olmoti halmashauri ya Jiji la Arusha mara baada ya wananchi kulalamikia maji yenye kemikali hatarishi kwa mimea na viumbe hai yanayotiririshwa kupitia mitaro inayotokea kiwandani hapo na kuingia katika makazi ya watu bila mafanikio kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano mfululizo.
"Kiwanda hiki pamoja na kujenga mtambo mpya ambapo pamoja na kuwepo kwake bado hali ya uchafuzi wa mazingira imeendelea kuwa mbaya na hivyo naagiza leo kiwanda hiki kisitishe shughuli zote za uzalishaji zinazopelekea uwepo wa maji taka"Alisema mhandisi Ledemta
Awali kabla ya maelekezo hayo meneja wa NEMC kanda ya kaskazini Lewis Nzali anasema kama taasisi wamejitahidi kutoa elimu na kufanya kaguzi za mara kwa mara katika kiwanda hicho bila mafanikio yeyote.
Kwa upande wake afisa mazingira wa kiwanda hicho mhandisi Harryson Rwehumbiza amekiri kupokea maelekezo hayo na kwamba kama kiwanda hakitakuwa na bajeti ya matengenezo zaidi ya mtambo huo itawalazimu kufunga kiwanda hicho.
Post A Comment: