Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick akitoa chanjo kwa mmoja wa watoto kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya chanjo duniani yaliyofanyika kimkoa Kata ya Iyumbu wilayani Ikungi mkoani hapa Aprili 24, 2023.
................................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKOA wa Singida unatarajia kuwachanja watoto wote
36,350 walio chini ya miaka mitano ambao hawakupata chanjo na watoto ambao
wanaendelea na ratiba za chanjo zao pamoja na chanjo ya UVIKO-19.
Hayo yamesemwa Aprili 24, 2023 na Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter
Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya
chanjo duniani yaliyofanyika kimkoa Kata ya Iyumbu wilayani Ikungi mkoani hapa.
Dk. Ludovick alisema maadhimisho hayo yanawalenga
watanzania wote kutambua umuhimu wa chanjo katika kukinga milipuko ya magonjwa
na hivyo kuzuia ulemavu na vifo vinavyozuilika hasa kwa makundi maalum kama
watoto wenye umri chini ya miaka mitano, watoto wa kike wenye umri chini ya
miaka 14 na kwa chanjo ya UVIKO 19 watu wazima kuanzia miaka 18 lakini hasa kwa
watoto wadogo zaidi na makundi yaliyotajwa hapo.
"Takwimu za utafiti wa magonjwa mengi ya
kuambukizwa yanayozuilika kwa chanjo huathiri zaidi watoto wadogo hasa wenye
umri chini ya miaka mitano, hivyo basi chanjo huwapatia kinga ya ziada dhidi ya
magonjwa hayo," alisema Ludovick.
Alisema pamoja na muitikio mkubwa wa wananchi
kwenye kampeni mbalimbali za chanjo, takwimu zinaonesha uwepo wa mlipuko ya
ugonjwa wa surua na Rubella katika Halmashauri za Wilaya za Ikungi, Itigi na
Singida DC hivyo kuonesha bado kuna haja kubwa ya kutoa elimu na kampeni za
mara kwa mara kwenye jamii juu ya umuhimu wa watoto kukamilisha chanjo
mbalimbali.
Dk.Ludovick alisema katika halmashauri hizo watu
takribani 150 walibainika kuwa na dalili za ugonjwa wa Surua Rubella na eneo la
Kata ya Iyumbu kupitia vijiji vya Msake na Iyumbu vilionekana kuwa na watoto
wengi ambao hawakupata dhidi ya Surua Rubella.
Aidha Dk.Ludovick alitumia nafasi hiyo kuipongeza
Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa kushirikiana na Ofisi ya
Rais-TAMISEMI kwa kuratibu maadhimisho hayo kitaifa.
Pia alitoa pongezi kwa kamati ya maandalizi
ya Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa maandalizi mazuri kwa
kushirikiana na Mdau wa Afya ndani ya Mkoa JHPIEGO kwa jitihada zao
zilizofanikisha uzinduzi wa maadhimisho hayo.
Dk. Ludovick alisema watalaam wa afya Mkoa wa
Singida wamejipanga vizuri, sio tu kutoa chanjo bali hata kutoa huduma nyingine
za afya zikiwemo kutoa elimu ya afya kuhusu umuhimu wa kumaliza chanjo kwa
watoto na madhara ya watoto kutokumaliza chanjo, uchangiaji wa damu salama,
afya ya uzazi, lishe, magonjwa sugu yasiyoambukiza kama vile kisukari na
shinikizo la damu,malaria na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Singida, Habibu
Mwinorya alisema malengo ya maadhimisho hayo ni kuwafikia watoto wote chini ya
miaka mitano na watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea katika chanjo za UVIKO
19 kwa kuwachanja watoto wote 36,350 walio chini ya miaka mitano ambao
hawakupata chanjo tangu mwaka 2019.
Alisema malengo mengine ni kuwachanja watoto wote
6,535 waliokosa chanjo chini ya miaka mitano tangu mwaka 2019 hadi sasa na
kuwapatia chanjo watoto wote waliopo katika ratiba zao za kliniki za kila mwezi
hasa za mwezi Aprili, 2023.
Aidha, Mwinorya alisema lengo lingine ni
kuhakikisha watoto wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambao hawajapata
ama kukamilisha chanjo dhidi ya UVIKO-19 wanachanja na watoto wote ambao
walichanja kipindi cha zoezi la pili lililofanyika Machi 24 na 30, mwaka huu
wanarudia kukamilisha kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayozuilika kwa
chanjo.
Alisema kufikia mwaka 2023 Machi Mkoa wa Singida umeongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma za chanjo kutoka vituo 218 mwaka 2021 hadi vituo 237 sawa na asilimia 89 ya vituo 266 vinavyotoa huduma za afya na hiyo ni kutokana na vituo vilivyojengwa katika Awamu ya Sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambapo kuna vituo vipatavyo 29 vinavyotoa huduma lakini havina majokofu ya chanjo.
Post A Comment: