Ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kufufua zao la mkonge ambalo ni moja ya mazao makuu ya kipaumbele, Serikali ipo mbioni kufufua Korona ya kuchakata mkonge wa wakulima wadogo iliyopo katika shamba la Kibaranga wilayani Muheza ambalo limerejeshwa kwenye umiliki wa Bodi ya Mkonge Tanzania na kuendeshwa na wakulima wadogo.
Hayo yamesemwa leo tarehe 02 Aprili, 2023 na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde alipotembelea shamba la Kibaranga na kukagua miundombinu ya maghala na mitambo chakavu ya shamba, ikiwa ni pamoja na kuzindua awamu ya pili ya ugawaji miche kwa wakulima wa mkonge inayotolewa bure na Bodi ya Mkonge Tanzania.
"Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuondoa changamoto ya upotevu wa mkonge mwingi wa wakulima wadogo kutokana na uosefu wa mitambo ya Korona kwa ajili ya kuchakata mkonge.
Napenda kuwajulisha wakulima wa Kibaranga kuwa, Mhe. Rais ametupatia fedha tayari ya ukarabati wa mashine hii ya korona, na tunakwenda kuifufua haraka ili ianze kuwahudumia na kuwapunguzia aza na gharama ya kwenda zaidi ya kilometa 100 kupata huduma ya kuchakata mkonge wenu”Alisema Mavunde
Sambamba na hilo, Mhe. Mavunde alibainisha kuwa Serikali inakamilisha hatua za mwisho za ununuzi wa mashine za Korona tatu (3) ambazo zitakuwa chini ya Bodi ya Mkonge kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji wa mkonge kwa wakulima wadogo nchini na kuondokana na tatizo la mkonge kuozea mashambani.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amezinduaa zoezi la ugawaji wa miche ya mkonge kwa wakulima nchi nzima na kubainisha kwamba Serikali inatoa miche hiyo bure na hivyo itahakikisha inafuatilia kila mkulima atakayechukua ili miche hiyo iwe na tija inayotarajiwa.
Kufuatua hatua hiyo Serikali imekuja na mfumo mpya utakaotumika kugawa miche ambapo miche yote tunayogawa tutaipa namba ya utambulisho na kusajili imechukuliwa na nani na kwenda kupandwa wapi, hii itasaidia zoezi la ufuatiliaji kuwa rahisi na kuongeza tija kwa fedha ya Serikali.
Awali, akitoa taarifa ya shamba hilo kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Bw. Sadi Kambona alieleza kwamba ikiwa sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la mkonge, Bodi imepanga kuzalisha miche bora milioni 6 kwa mwaka wa fedha 2022/23 na kuisambaza kwa wakulima nchi nzima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mheshimiwa Juma Irando alimweleza Naibu Waziri kuwa ataendelea kushirikiana na Bodi ya Mkonge kuhakikisha wanaendelea kutatua changamoto za wakulima na kuendeleza zao la mkonge ili linufaishe wakulima wa Muheza na Taifa kwa ujumla.
Post A Comment: