Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo akikagua hali ya mazingira ya kituo cha afya cha Namatula ambako hakuridhishwa na hali ilivyo ya kimazingira.


Na Fredy Mgunda, Nachingwea.


WANANCHI wanaopata huduma katika kituo cha afya Namatula wamelalamika kuwa wapo mbioni kupata magonjwa mengine ya mlipuko kutokana uchafu wa mazingira yanayokizunguka kituo hicho cha afya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo, baadhi ya wananchi walisema kuwa serikali imejenga majengo mazuri na mengi lakini hali ya usafi bado tete.

John Sangawe ni mmoja ya mwananchi alisema kuwa majengo yamejengwa kwa ubora unaotakiwa na huduma zinazotolewa vizuri tatizo kubwa kituo hicho kimekuwa kama pori na kina madimbwi mengi ya maji ambayo sio sawa kwa wagonjwa na wananchi wanaoenda kupata huduma za afya hapo.

Sangawe alisema kuwa madimbwi na majani mengi yanaweza kuzalisha ugonjwa kama malaria au mwananchi anaweza kung'atwa na nyoka kutokana eneo la kituo cha afya cha Namatula kuwa na vichaka vingi.


Agata Ngeyesa alisema kuwa anauomba uongozi wa kata ya Namatula kuhakikisha wanafyeka nyasi zote kwenye kituo hicho cha afya na kuyaondosha madimbwi yote ambayo yapo katika kituo hicho cha afya.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo alikiri kuwepo kwa madimbwi ya maji pamoja na nyasi nyingi ambazo zinaweza kusababisha magonjwa mengine kwa wananchi na wagonjwa wanaotaka kupata huduma ya afya hapo.

Moyo aliugiza uongozi wa kata na kituo cha afya cha Namatula kuhakikisha wanafanya usafi na kukifanya kituo hicho cha afya kuwa Safi kulingana na hadhi ya majengo yaliyopo.

Aliagiza kuhakikisha vituo vyote vya afya vinafanya usafi kila Mara ili kulinda afya za wagonjwa na wananchi wanaenda kupata huduma katika vituo hivyo vya afya.

Naye diwani wa kata ya Namatula George Kasembe alikiri kuwepo kwa madimbwi na majani mengi katika kituo hicho cha afya na kuahidi kufanya usafi mwishoni mwa wiki kwa siku mbili mfululizo.

Dkt David Bryson Mkileja ni Mganga mkuu wa kituo cha afya cha Namatula alikiri kuwepo kwa madimbwi na majani mengi katika kituo hicho na kumuahidi mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo kulifanyia kazi Jambo hilo na kukiweka kituo cha afya katika hali nzuri ya kimazingira kuendana na hadhi ya majengo.


Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: