Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameshukuru juhudi za wafanyabiashara Kisiwani Pemba katika kutoa huduma na kukabiliana na changamoto za bei ya bidhaa kwa wananchi, ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mheshimiwa Othman ametoa shukran hizo leo, alipowatembelea wafanyabiashara wa bidhaa mbali mbali, huko Masoko ya Chakechake na Wete, katika Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba.
Amesema shukrani hizo zimetokana na ubainifu kwa baadhi ya wauzaji kuzingatia uwiano baina ya tija ya biashara na ulazima wa tunu za baadhi ya bidhaa miongoni mwa wananchi, hasa katika Msimu huu wa Funga.
"Nawashukuru sana kwani nia yetu sote ni kuhakikisha tunakabiliana na changamoto ya bei kwa baadhi ya bidhaa hasa zile ambazo zinawalazimu wananchi wakati huu wa Ramadhan", amesisitiza Mheshimiwa Othman.
Hivyo amewataka wafanyabiashara, viongozi, pamoja na wananchi kuonyesha mashirikiano ili kuhakikisha kunakuwepo na unafuu wa bidhaa, utakaopelekea kukidhi mahitaji na hatimaye kuwepesisha maisha, hasa ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mheshimiwa Othman, ambaye amewatakia Waislamu wote 'Ramadhan Kareem', akiambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, amewasili leo kisiwani Pemba kwa Ziara Maalum, na kupokelewa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Dini, Vyama vya Siasa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi Salama Mbarouk, amepongeza mwitikio wa sasa wa wananchi kwa Serikali yao, huku akikaririwa akisema, "ukweli ni kwamba kumekuwepo na uzito wa upatikanaji wa baadhi ya bidhaa zikiwemo ndizi kutokana na kusafirishwa kwenda nje ya Pemba".
Nao, miongoni mwa wafanyabiashara katika Masoko hayo, Bw. Iddi Ali, Bi Sada Rashid na Bw. Said Mbarak wameeleza kuwa licha ya kuwepo athari za Kiangazi katika mavuno ya Mwaka huu, wanafanya kila juhudi kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa tunu kisiwani hapa, zikiwemo Muhogo wa Gando, Ndizi za Vikunguni, Viazi vya Msuka, Nazi za Wingwi, Samaki, Duvi na Dagaa la Wesha na Majimbi kutoka Mikarafuuni Mkoani.
Viongozi mbali mbali wameambata na Mheshimiwa Othman katika Ziara yake hiyo, wakiwemo pia Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Bw. Mattar Zahor Masoud, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, na Mratibu wa ACT-Wazalendo Kisiwani hapa, Mhe. Said Ali Mbarouk.
Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Jumatatu, Aprili 3, 2023.
Post A Comment: