Na Denis Chambi, Tanga.
MWENYEKITI wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe ametoa mapendekezo kwa vyama vyote vya siasa hapa nchini kuunda tume ya kitaifa itakayohusika kusimamia na kuangazia maswala haki na ukweli hii ikilenga kufanya uchunguzi na kuondoa utengano wa kimaslahi kupitia nyanja mbalimbali kwa maslahi mapana watanzania.
Akizungumza mkoani Tanga katika mkutano wa hadhara na wanachama wa chama hicho march 8, 2023 Zitto alisema kuwa licha ya michakato mingi ya kisiasa inayofanyika hapa nchini kila chama kikisimamia sera zake kuna haja ya kuunda tume mahususi kwajili ya kuangazia haki na ukweli itakayo kuwa na lengo la kutatua changamoto mbalimbali za kisiasa zilizojitokeza na zitakazojitokeza kwa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa ambapo wengi wanaweza kungia katika migogoro katika harakati za kutafuta haki zao.
"Tumekuwa tukisistiza kwamba kuna haja nchi yetu iwe na tume ya haki na ukweli ili kila mtu ambaye aliumizwa kwa namna yeyote ile aweze kupata msaada wakiwemo waliozushiwa kesi yeyote, waliofungwa kwa makosa mbalimali yakiwemo ya jinai na mengineyo haya yote yanahitaji tuwe na tume ya uchunguzi ambayo iyayatazama mambo haya ili wale ambao walionewa na kunyang'anywa mali zao, makosa ya jinai wafutiwe makosa yao hapo ndipo tunaweza kusema nchi inapona hatuwezi kuiponya nchi hii kwa kufunika mambo" alisema Zitto.
Pamoja na hayo chama hicho cha ACT Wazalendo kimeitaka serikali kuangalia upya suala la mswada wa Bima ya afya kwa wote ambao ulishindwa kupitishwa na muhimili wa Bunge kutokana na kutoridhishwa nao ikiwemo gharama zinazotakiwa kuchangia ambapo bado kimeona kuwa itakuwa ni mzigo mzito kwa wananchi.
Alisema kuwa kupitishwa kwa mswada huo bado serikali itakuwa haijamsaidia mwananchi kutokana na gharama kuwa kubwa licha ya hali ya kipato chake kuwa chini ambapo kila mwananchi anapaswa kuchangia kiasi cha shilingi laki tatu na elfu arobaini (340, 000) kwa mwaka.
"Mswada ambao serikali imeupeleka ili kutunga sheria ya bima ya afya ni mswada ambao utaendelea kutukalisha watanzania kwa sababu ni mswada ambao unaiondoa serikali kwenye jukumu lake la kushughulikia na kuhudumia wananchi wake inapeleke mzigo ule kwenu wananchi na huku serikali haichangii chochote"
"Wazo letu sisi tunataka serikali ichangie kwenye gharama za afya ambazo watanzania wanagharamia hatutaki ijitoe kwenye mfumo wa bima ya afya kama ambavyo serikali inawachangia pensheni watumishi wa umma ndio hivyo hivyo tunataka mwananchi ambaye anachangia kwenye bima ya afya ndio maana tunasema tunataka Taifa la wote maslahi ya wote" aliongeza Kiongozi huyo
Katibu mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Ado Shaibu ameipongeza serikali ya awamu ya 6 ya chama tawala chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya kufanyika kwa mikutano ya kisiasa nchini mara baada ya kufungiwa kwa mika kadhaa iliyopita hatua ambayo imeonekana kuleta matumaini mapya kwa watanzania kupitia vyama mbalimbali.
"Tangu uchaguzi mkuu umalizike mwaka 2020 sisi ACT Wazalendo tulijitahidi kupambana kuhakikisha tunaongoza njia katika mageuzi ya msingi ya kisiasa Tanzania, kabla ya serkali ya awamu ya 6 kuingia madarakani sisi tulichukua hatua ya kukubali kushiriki mazungumzo ya kisiasa tuliona umuhimu wa maridhiano ya kitaifa tunaamini usipoongoza utaongozwa, " alisema
Aidha katibu huyo alisema kuwa harakati za chama hicho kupitia mikuano walitoshiriki na vyama vya siasa ilivyofanyika hapa nchini licha ya kuonekana matokeo chanya na maridhiano bado hakikusita kueleza umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya itakayoleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali ikiwemo za kiuchumi, kibiashara na kijamii huku akipendekeza kuwepo na mkutano wa kitaifa wa kikatiba utakaosaidia kupatikana kwa katiba mpya.
"Tumeshiriki mazungumzo mbalimbali yaliyoitishwa na baraza la vyama vya siasa Tanzania , tumeshiriki pia mazungumzo yaliyoitishwa na kituo cha demokrasia Tanzania kila mahala tulisema kwamba ili nchi hii ipone kisiasa kiuchumi na kijamii tunahitaji katiba mpya na hatujaishia tu kwenye katiba mpya bali tumeeleza kuanzia marekebisho ya kisheria zinazoongoza mchakato wa katiba mpya "
Awali akizungumza makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Tanzania bara Doroth Temu alisema bado suala la kukosekana kwa chakula cha kuyosha na kupanda kwa bei za vyakula hapa nchini imekuwa ni maumivu kwa wananchi wa hali za chini hali ambayo inaweza kuchangia wengi wao kushindwa kumudu gharama za vyakula akiiomba serikali kuendelea kutafuta suluhisho kwa mslahi mapana ya watanzania.
"Tunaingia msimu wa kilimo lakini bado bei za vyakula zipo juu sana, kila tunapopita hilo limekuwa ni kilio kwa wananchi wote, Suala la njaa wasilifanyie dhihaka, wananchi wa kipato cha chini wana maisha magumu mno uwezo wa Taifa kulisha watu wake kupata uhakika wa kupata chakula kwa bei nzuri ni suala nzuri katika ujenzi wa Taifa serikali bado haijaja na majibu ambayo yanamsaidia mwananchi wa kawaida kweli bei ya chakula imepanda na gharama zimekuwa maumivu" alisema Doroth.
" Sisi tumependekeza kwa serikali kama suluhisho la muda mrefu tuhakikishe tunawawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa kuwapatia pembejeo kwa bei nafuu ili hawa wakulima waweze kuzalisha chakula kingi zaidi lakini tunafahamu serikali imetoa kibali cha kuagiza tani elfu 90 za mchele hivyo kama suluhisho la muda mfupi tunaitaka serikali ihakikishe kwamba chakula kinapofika nchini kinagawanywa na kusambazwa kimfikie mtu wa kawaida kwa bei nafuu" alisistiza
Aliongeza kuwa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya kila halmashauri ambazo o hutengwa ili kuyawezesha makundi ya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu bado kuna malalamiko ya kuwepo kwa mlolongo mrefu wengi wao wakishindwa kupata fedha hizo kwa wakati na hatimaye huhutana na na kushibwa kuchangia pato la Taifa.
" Wanawake wanalia mikopo tumesikia sasa hivi kuna mikopo ya kausha damu , wanawake wanahitaji kuwezeshwa wapate mikopo yenye riba nafuu , hii mikopo wengi wamekuwa wakiihangaikia lakini hawaipati kutokana na mchakato kuwa mrefu ni wakati sasa wa kuhakikisha kwamba tunawapunguzia wanawake mateso ya kupata mitaji ikiwemo kila mwanamke angalauaweze kupata huu mkopo wa halmashauri usio kuwa na riba ili naye aweze kuchangia katika pato la Taifa." alisema
Baadhi ya wanachma wa chama cha ACT Wazalendo wakifwatilia hotuba ya kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe katika mkutano wa hadhara uliofanyika March 8, 2023 kwenye uwanja wa Tangamano jijini Tanga.
Post A Comment: