Na Joachim Nyambo,Mbeya.
TAASISI
ya WeCare kwa kushirikiana na Hospitali ya Aghakhan wamefungua kituo
cha Maendeleo ya awali ya mtoto kitakachotumika kutoa mafunzo kwa wazazi
na walezi wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano juu ya
Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(MMMAM) hospitalini hapo.
Kuanzishwa
kwa kituo hicho ni sehemu ya Taasisi binafsi kuunga mkono juhudi za
serikali kwenye utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi,
Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) inayoendelea
kutekelezwa katika mikoa kumi nchini ukiwemo Mkoa wa Mbeya.
Akimwakilisha
Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya,Dk Jonas Lulandala kuzindua kituo
hicho,Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto jijini hapa, Aquina Mtweve
alipongeza hatua ya taasisi hizo kuamua kuwekeza kwenye ukuaji wa awali
wa mtoto hatua aliyosema inalenga kuwezesha kuwa na taifa lililo na
rasilimali watu walio na ukuaji timilifu hapo baadaye.
Mtweve
aliwataka wazazi na walezi kutambua kuwa kinachofanywa na serikali na
wadau katika kusimamia ukuaji sahihi wa mtoto si maigizo bali kuna faida
kubwa hivyo ni muhimu kwao wakawa tayari kupokea yale yanachofundishwa
na wataalamu na kuyafanyia kazi majumbani.
“Tumeona
hapa mwalimu alipotuonesha namna ya uchangamshaji watoto kupitia
michezo… unaweza ukaona kama ni maigizo au ni mchezomchezo tu…lakini huu
ndiyo msingi muhimu sana wa ukuaji wa mtoto… Wazazi na walezi haya
ndiyo tunapaswa kuyafanya majumbani ili kuwajenga watoto kuwa na ukuaji
timilifu.” Alisisitiza Mtweve.
“Tunafurahi
kuona kituo hiki ambacho ni cha kwanza hapa mkoani kwetu kinafunguliwa
katika jiji letu. Tunajua kwamba katika Mkoa wa Mbeya, jiji ndilo
linabeba idadi kubwa ya wakazi hivyo tukifanikisha hapa tutafanikiwa
kimkoa pia.” Aliongeza.
Hata
hivyo Mratibu huyo wa Afya ya Uzazi na mtoto alishauri Taasisi husika
na wadau wengine kuona uwezekano wa kufungua vituo vingine kama hivyo
kwakuwa uhitaji ni mkubwa.
Kwa
upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tasisi ya WeCare, Elizabeth Magunga
alisema walifikia uamuzi wa kufungua kituo hicho baada ya kuona watoto
waliokuwa wakiwapokea kwenye kituo chao cha malezi ya awali ya mchana
wakiwa na mapungufu mbalimbali ya ukuaji kutokana na wazazi kukosa
uelewa wa kutosha juu ya namna sahihi ya kumsaidia mtoto kupitia ukuaji
timilifu.
Magunga alisema
kupitia kituo hicho sasa wazazi watakao kuwa wakihudhuria kliniki
katika Hospitali ya Aghakan na wale watakao fika siku atakazopanga
daktari wa watoto hospitalini hapo watapata wasaa wa kukutana na
kujifunza kutoka kwa wataalamu wa MMMAM.
Aliyataja
maeneo makuu matano yatakayozingatiwa kwenye utoaji elimu kwa wazazi
kupitia kituo hicho kuwa ni pamoja na Afya, Lishe bora, Malezi yenye
muitikio, Ulinzi na Usalama pamoja na Ujifunzaji wa awali.
Naye
Meneja wa Hospitali ya Aghakhan tawi la Mbeya,Michael Mwanisenga
alisema uwepo wa kituo hicho utaisaidia pia jamii kuondokana na baadhi
ya maradhi yanayowakabili watoto yanayotokana na wazazi na walezi kukosa
uelewa wa kutosha wa namna ya kuwakinga watoto wao ikiwemo udumavu na
utapiamlo.
Mwanisenga
aliwakaribisha wadau wengine walio na utayari wa kushirikiana na
hospitali hiyo kwenye uwekezaji unaoweza kuisaidia jamii akisema lengo
ni kuona kunakuwa na ustawi kwenye jamii kwa kuepuka maradhi hususani
yanayohatarisha maisha ya watoto.
Post A Comment: