Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Omary Mchengerwa, amewataka watendaji wa Wizara hiyo kuongeza ubunifu katika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi akitaka kuvuka lengo la kuleta watalii milioni 5 ifikapo 2025.
Mhe, Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa kufungua kikao cha 30 cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo mjini Dodoma leo kilichohudhuriwa pia na Naibu Waziri, Mary Masanja, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, na Naibu Katibu Mkuu, Anderson Mutatembwa.
Amezitaja njia ambazo zinapaswa kutumiwa na Wizara ili kufikia azma hiyo kuwa ni pamoja na kuimarisha utalii wa uwindaji wa wanyamapori, kukuza utalii wa mikutano na kuendeleza utalii wa fukwe.
Pia kuendelea kujenga uwezo wa wadau katika kusimamia rasilimali za wanyamapori, misitu na nyuki na kuendelea kudhibiti ujangili wa wanyamapori na mazao ya misitu na nyuki.
Aidha, kusimamia, kuendeleza na kulinda malikale kwa manufaa ya Taifa.
Amezitaka Taasisi za Wizara kujikita katika kuhifadhi raslimali pia kuja na mikakati mipya ya kubuni mazao mapya ya utalii ili kuwafanya watalii kuwa na siku nyingi za kukaa nchini baadala ya kutegemea utalii wanyamapori pekee.
Kufuatia hatua hiyo ametaka vivutio vya utalii vilivyoko katika Mkoa vinatambuliwa na kusisitiza kuwa zoezi litakwenda hadi katika ngazi za wilaya ili kuhakikisha vivutio hivyo vinaainishwa na kutangazwa kimkakati ili kujulikana dunia kote.
Amesema ni wakati muafaka sasa sekta ya utalii kuifanya agenda ya kitaifa kwa kuhamasisha Watanzania wanatembelea vivutio vya utalii.
Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi, Mhe.Mchengerwa amesema atahakikisha yanapewa kipaumbele huku akimuelekeza Katibu Mkuu kuhakikisha madeni ya Watumishi yanalipwa kwa wakati ili waweze kufanya kazi kwa moyo
"Tunataka kuona nyuso za furaha kwa watumishi wa Wizara hii" Amesisitiza Mhe.Mchengerwa
Aidha, Amewataka Viongozi wa Wizara kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya Watumishi kwa wakati
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja ametoa wito kwa Watumishi kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili kuhakikisha azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhifadhi raslimali na kutangaza vivutio vya utalii duniani inatimia.
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas amefafanua katika Mkutano huo kwamba awali Wafanyakazi wameweka maazimio mengi likiwemo la Watumishi kupewa mafunzo kila wakati kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi baadala ya kusubiria wakati wakielekea kustaafu.
Pia ameyataka Mabaraza ya Wafanyakazi yatumike kutoa elimu mbalimbali zenye tija kwa wafanyakazi ikiwa ni pamoja na masuala ya kustaafu utumishi ili waanze kujiandaa mapema.
Post A Comment: