Watumishi 12 wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Mkoani Arusha wametakiwa kukaa pembani kupisha uchunguzi wa tuhumiwa ya ubadhilifu wa zaidi ya shilingi milioni 150 wakiwemo wakuu wa idara nne ambao tayari wametelemshwa vyeo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi{CCM} iliyosomwa na Katibu Mwenezi wa Chama, Solomoni Lekui na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Saimon Oitesoi ilisema kuwa hatua hiyo ni kufuatia taarifa ya ukaguzi ya mwaka 2021.
Lekui aliwaeleza waandishi Habari kuwa mbali ya ubadhilifu watumishi hao walikuwa wakifanya mambo kinyume na utaratibu na kutumia vibaya madaraka yao walipokuwa kazini hivyo waliomba mamlaka husika ziweze kuchukuwa hatua dhidi yao ili iwe fundisho kwa wengine.
Katibu huyo alisema kuwa chama kiko katika kusimamia,kuelekeza na kukemea watumishi wanaokwenda kinyume na taratibu na kamwe chama hakiwezi kukaa kimya na kuona mambo yanakwenda hovyo hilo halitawezekana.
‘’Tunaomba Mamlaka husika ziweze kuwachukulia hatua wale wote waliotajwa katika ripoti hiyo kwa ubadhilifu wa mamilioni ya pesa Longido’’alisema Lekui
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido ,Stephen Ulaya Alisema kuwa hatua za awali zimeshachukuliwa kwa Wakuu wa Idara nne ambao wameshushwa vyeo na kupangiwa kazi nyingine na hatua zingine zikifuata baada ya uchunguzi kukamilika.
Ulaya alitaja Wakuu wa Idara ambao wameshushwa vyeo ni pamoja na Idara ya Ugavi na Manunuzi,Ujenzi,Mapato na Biashara ambao wamepangiwa kazi nyingine.
Alisema watumishi wengine ambao wanadaiwa kutuhumiwa na ubadhilifu,matumizi mabaya ya ofisi na ukiukwaji wa taratibu uchunguzi bado unaendelea na ikibainika hatua Zaidi zitachukuliwa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longido,Saimoni Oitesio alipoulizwa juu ya ubadhilifu huo na yeye kwa nini ameshindwa kusimamia alisema kuwa kushindwa kusimamia sio kweli kwani yuko katika kulinda fedha za Umma bila kumwonea mtumishi.
Oitesio alisema kuwa na ndio maana baadhi ya wafanyakazi wamesimamishwa kazi na wengine wametolewa katika kuongoza idara hiyo ni hatua dhidi ya watumishi wenye kula fedha za Umma na bado wengine wanachunguzwa.
Akizungumzia yeye kuhusika katika zabuni kupitia gari yake,Mwenyekiti huyo alisema sio za kweli kwani gari yake aliikodishia kwa mtu binafsi kufanya kazi ya Halmashauri ya sio yeye kufanya kazi hiyo kama inavyodaiwa na watu na kusambazwa katika mitandao ya kijamii.
Mwenyekiti alisema aliikodisha gari hiyo mwaka jana kwa mtu binafsi na sio mwaka huu na mwaka wote huu gari hiyo ameipaki nyumbani kwake.
Alisema na kuwataka watumishi wa Halmashauri kuwa atakuwa rafiki wa mtumishi anayefuata taratibu na kamwe hatamwacha salama mtumishi anayekula fedha za Umma kwani huyo atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria.
‘’Niko hapa kuhakikisha kila kitu kinafuata sheria na taratibu na taarifa zote za ubadhilifu lazima zifanyiwe kazi kwa maslahi ya Umma’’alisema Oitesoi
Post A Comment: