Na John Walter-Hanang’
Kutokana na malalamiko ya baadhi ya madereva wa magari ya mizigo kuibiwa mizigo wanapopita katika kijiji cha Masakta wilayani Hanang’ mkoa wa Manyara, uongozi wa kijiji hicho kwa kushirikiana na wananchi wamewasaka na kuwakamata vijana wanaodaiwa kujihusisha na uhalifu huo.
Wananchi wamesema wamewakamata vijana sita wanaotajwa kuhusika na matukio hayo ya wizi.
Serikali wilayani humo kupitia mkuu wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Janeth Mayanja amepongeza hatua zilizochukuliwa na wananchi hao na kuwahakikishia madereva wa magari ya mizigo kwamba usalama upo.
Mayanja amesema hawezi kumvumilia yeyote anayechafua wilaya ya Hanang’ kwa vitendo vya kihalifu na kwamba watashughulika na wahusika wote.
Amelitaka jeshi la polisi lisikate tamaa kuwasaka wahalifu hao na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili kurejesha Amani ya Masakta.
Hata hivyo amewaondoa hofu madereva wa malori ya mizigo wanaopita katika wilaya hiyo kwenda maeneo mbalimbali ya nchi kuwa kwa sasa hali ni shwari.
Wengine wamesema kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kijiji wanawaunga mkono wahalifu hao kwa kuwa wanakutana na kunywa pamoja pombe.
Mmoja wa madereva wa mizigo ambaye hakutaja jina lake amebainisha yeye aliwahi kuibiwa akiwa Singida na kwamba hasara yote iliyojitokeza alilazimika kuilipa kwa bosi wake na mbinu anayotumia kwa sasa ni kuweka miba nyuma ya gari.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kupora mizigo kwenye magari hayo yanayopita katika kata hiyo kwa kupanda juu wakati gari likendelea kutembea na kushusha mizigo kwa nyuma bila dereva wala utingo wake kujua.
Post A Comment: