Na WAF- SINGIDA
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewaagiza Wakandarasi kutoka kampuni ya Luba, MUST na Ardhi ambao waligomea wito wake wa kufika katika eneo la mradi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kufika kwa Mkuu wa Mkoa huo ili kujieleza kwanini mradi huo haumaliziki ndani ya wakati licha ya kulipwa fedha zote na Serikali.
Dkt. Mollel ametoa maagizo hayo leo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, pamoja na kukagua hali ya ubora wa huduma katika hospitali hiyo katika eneo la upatikanaji wa huduma za dawa.
Amesema, Wakandarasi kutoka Kampuni ya Luba, MUST na Ardhi wamegoma kuja katika eneo la ujenzi licha ya kutoa maelekezo wawepo katika eneo la ujenzi wa mradi ili kujadili kwa pamoja changamoto zinazowafanya kushindwa kutekeleza makubaliano ya kumaliza mradi ndani ya wakati licha ya kupewa fedha zote.
"Tumekubaliana na Mkuu wa Mkoa tutaenda nao hawa wawakilishi mpaka watapopatikana huyu muhusika wa Luba, pamoja na watu wa MUST na chuo cha Ardhi, waje Singida ili na wao wapate nafasi ya kusikilizwa, watuambie shida ni nini na kwanini kazi waliyopewa hawajaifanya kwa wakati."
Amesema kuwa, Mkandarasi kutoka Luba alitakiwa kumaliza mwezi Julai 2022, lakini hakutimiza makubaliano hayo licha ya kuongezewa muda mpaka Novemba 2022 wakati huo Serikali ikiwa imetimiza jukumu lake la kutoa kiasi chote cha fedha kwaajili ya mradi huo.
Aidha, Dkt. Mollel amesema wengine ambao hawajatimiza maelekezo ya kufika katika eneo la ujenzi wa mradi ni taasisi ya MUST pamoja na Chuo cha Ardhi, huku akisisitiza wote watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Utumishi wa umma.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na kuwataka waongeze juhudi katika utoaji huduma licha ya kuwa moja kati ya hospitali zilizofanya vizuri katika eneo la utoaji huduma hasa eneo la vifo vya wajawazito.
Pia, amewaelekeza Wataalamu kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa kuwajengea uwezo na kuwasimamia hospitali ya Wilaya ili zikasimamie vituo vya afya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Post A Comment: