Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema Serikali inadhamira thabiti pamoja na washirika wa maendeleo kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 1,035.23 sawa na Dola za Marekani milioni 442.4 ili kutekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira hapa nchini.
Mhe. Mahundi amesema hayo akifungua Mkutano wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Maji ambayo pia ni Siku ya Maji Duniani.
Amefafanua uwekezaji huo uliofanyika kati ya Januari hadi Desemba 2022 umeongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kufikia asilimia 77 vijijini na asilimia 88 mijini na kusisitiza lengo ni kufikia asilimia 85 vijijini na mijini asilimia 95.
“Tunataka pia kufikia lengo la sita la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa wote ifikapo2030” Mhe. Mahundi amesema na kuongeza kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali za maji zinazokadiriwa kufika mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka, zinazojumuisha mita za ujazo bilioni 105 juu ya ardhi na mita za ujazo bilioni 21 chini ya ardhi.
Ameongeza kuwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi , Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa madogo na ya kati katika Bodi zote za maji za mabonde tisa.
Hatua nyingine, ameainisha ni pamoja na Serikali kutoa fedha za kuendeleza visima vilivyochimbwa katika maeneo ya Kimbiji na Mpera na kutumika kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji katika jiji la Dar es salaam na mkoa wa Pwani. Pia, ujenziwa bwawa la Kidunda umeanza ili kuhakikisha upatikanaji wa majiendelevu jijini Dar es salaam.
Mhe. Mahundi amedokeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeanza maandalizi ya ujenzi wa bwawa la Farkwa ili kuhudumiajiji la Dodoma.
Amesema suala la kuendeleza rasilimali za maji chini ya ardhi Serikali imelipa kipaumbele na kupitia mfuko wa COVID 19 mitambo ya kuchimba visima seti 25 na vifaa vya ujenzi wa mabwawa seti tano vimenunuliwa.
Awali, akiongea kuhusu Siku ya Maji Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema Wizara ya Maji imejipanga kuwa na mfumo wa mtandao wa maji wa Taifa (Grid) utakaotoa maji katika maeneo yenye maji mengi ili kupeleka katika maeneo yenye upungufu wa maji.
Leo Machi 22 ni Siku ya Maji Duniani ikiwa na Kaulimbiu ya maadhimisho “Kuongeza Kasi ya Mabadiliko katika Sekta ya Maji kwa Maendeleo Endelevu ya Uchumi”
Post A Comment: