Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga ameitaka Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo (FADev) kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ili Serikali na jamii itambue kazi zinazotekelezwa na taasisi hiyo.

Rai hiyo, imetolewa Machi 22, 2023 alipokutana na Uongozi wa taasisi ya FADev ambao umefika kwa lengo la kujitambulisha na kueleza majukumu yanayofanywa na taasisi hiyo Kuendeleza Uchimbaji Mdogo katika kikao kilichofanyika ofisi za wizara Mtumba jijini Dodoma.

Dkt. Mwanga ameitaka FADev ishirikiane na Serikali ili kujenga mahusiano mazuri katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali na kusaidia kuepusha kuingiliana na majukumu hayo mara kwa mara.

Aidha, ameitaka FADev kuendelea kuilinda taasisi hiyo kwa kuheshimu taratibu na misingi iliyowekwa na nchi ambayo inalinda utu wa watanzania katika majukumu yao.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa FADev Mhandisi Theonestina Mwasha amesema kuwa, inaendelea kutekeleza miradi inayokuza na kuimarisha uzalishaji wa dhahabu katika mikoa ya Geita na Shinyanga.

“Tunafanya mafunzo katika maeneo ya uchimbaji, tunatoa elimu shirikishi kwa jamii inayozunguka migodi nakuanzisha mchakato wa kutoa elimu ya kuongeza thamani kwa ushirikiano wa wadau,” amesema Mhandisi Mwasha.


Akizungumzia kuwaendeleza wachimbaji wadogo Mhandisi Mwasha amesema, taasisi imetoa vifaa vya uchimbaji migodi kwa vikundi mbalimbali walivyofanya navyo kazi sambamba na kuimarisha vikundi vya wanawake 15 katika mikoa ya Geita na Shinyanga.

Amesema, hadi sasa taasisi ya FADev imefanikiwa kutoa mbinu za ujasiriamali kwenye maeneo ya uchimbaji madini, mafunzo ya utunzaji wa mahesabu, mafunzo ya ukusanyaji na utunzaji wa taarifa na matumizi sahihi ya kemikali zinazotumika kwenye uchenjuaji.

Pia imefanikiwa kutoa mikopo isiyozidi milioni 15 kwa kila kikundi kwa vikundi vitatu kwa kushirikiana na benki ya NBC.

Kikao hicho, kimehudhuriwa na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).


Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: