Na John Walter-ManyaraLicha ya ukame kukumba maeneo mengi nchini na wananchi kuwa na hofu kutokana na mazao yao kufa, serikali imesema nchi ipo salama kwa kuwa kuna chakula cha kutosha kilichohifadhiwa.
Hayo yamesema na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Bonga Halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara akipita kuelekea mkoani Arusha.
Simbachawene amesema Nchi ipo salama na kuwahakikishia Watanzania kuwa katika serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan hakuna atakayekufa kwa njaa.
Amesema wameanza na mahindi ya bei rahisi ili waweze kushusha wale wanaopandisha masokoni, na kwamba kila mahali wamepeleka Mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na watazidi kuongeza zaidi ili bei ishuke na wananchi waweze kumudu.
"Hata hivyo bado Rais ana nguvu, hata wale watakaozidiwa bado anaweza kusema wasaidiwe, anaweza kusema masikinini wapewe bure na chakula hicho kipo, lakini kwa sasa tumeanza kutoa kile cha kupunguza makali ya bei" alisema Simbachawene
Naye Naibu waziri wa Katiba na Sheria Paulina Gekul (Mbunge wa Babati mjini) amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi katika wilaya ya Babati njaa ipo na mahindi ni bei ghali ambapo kwa debe moja ni kuanzia shilingi 22,000 hivyo kupitia msaada huo uliotolewa na Rais Samia itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makali ya maisha wakati wananchi wakiendelea kusubiri mvua.
Nao wananchi wameishukuru serikali kwa msaada huo huku wakiomba punguzo kutoka shilingi 800 kwa kilo ya sasa hadi kufika shilingi 700 au hata 600 wakidai kuwa baadhi yao hawana uwezo kabisa.
Post A Comment: