Muonekano wa sehemu ya barabara ya Sanzate – Nata (km 40), inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Mara.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Nyamuswa – Bulamba (km 56.4), iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya takribani Bilioni 67 mkoani Mara. Barabara hiyo ni kiungo muhimu kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na Mikoa ya Kaskazini pamoja na Kisiwa cha Ukerewe.Serikali imewahakikishia wananchi wa Isenye, Wilaya ya Serengeti kuzimaliza changamoto zinazoukabili mradi wa ujenzi wa barabara ya Nata - Sanzate (km 40) kwa kiwango cha lami ili iweze kukamilika na kuondoa adha ya usafiri wanayoipata wananchi hao.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akijibu maswali ya wananchi na kuahidi kutoa ushirikano kwa mkandarasi kwa kuonesha maeneo yote yenye changamoto ili yaweze kutatuliwa kwa haraka pindi ujenzi wa barabara hiyo unapoendelea.
Wananchi hao wameeleza changamoto hizo kuwa ni pamoja na kusuasua kwa mradi na mkandarasi kutoweka mifereji ya kupitisha maji na hivyo kuathiri makazi ya watu.
"Siku zote unapohitaji maendeleo lazima kutakuwa na mabadiliko mengi ya utaratibu wa maisha yaliyokuwepo, na uwepo wa ujenzi wa barabara hii si kukomoa au kuonea watu bali ni kuleta manufaa makubwa na endelevu kwa jamii”, amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya
Aidha, amemuagiza mkadarasi kuongeza vifaa, rasilimali watu na kuongeza muda wa kazi hata kwa kufanya kazi usiku na mchana kwa kuwa wananchi wanahitaji kuona barabara hiyo ikiwa imekamilika.
“Tumemuagiza aongeze wafanyakazi, vifaa na ikiwezekana aongeze shift ili barabara hii ikamilike na ndio kilio cha wananchi hawa kuona barabara inakamilika”, amesema Eng. Kasekenya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Vicent Mashinji, amemshukuru Naibu Waziri Kasekenya kwa ujio wake katika mkoa huo kwani utaleta msukumo katika ujenzi wa miradi mingi inayoendelea hasa kwa barabara hiyo kwani ni kiungo muhimu kati ya Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini na nchi jirani ya Kenya.
Akijibu hoja ya wananchi kuhusu uwepo wa mifereji, Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) mkoa wa Mara, Eng. Vedastus Maribe, amesema changamoto hiyo anaifahamu na amekwisha muelekeza mkandarasi kusambaza vifusi vilivyowekwa katika maeneo hasa ya makazi ili kuzuia athari za maji kuingia ndani ya nyumba za watu.
Kuhusu mradi wa barabara hiyo, Eng. Maribe, ameeleza kuwa mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 32 na kazi zinazoendelea ni pamoja na kunyanyua tuta la barabara ambapo hadi sasa mkandarasi kafikisha km 23.4 na pia amekwishajenga madaraja madogo 45 kati ya 46, madaraja 11 kati 16 na madaraja makubwa kashajenga 1 kati ya 2 yanayotakiwa.
Ameeleza ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa gharama ya takribani Bilioni 39 na mkandarasi China Railway Seventh Group na kusimamiwa na Kitengo cha Usimamizi wa Miradi cha Wakala ya Barabara nchini (TANROADS) – TECU.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amekagua na kuridhishwa na barabara ya Nyamuswa hadi Bulambwa (km 56.4) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya takribani Bilioni 67 zote zikiwa ni fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mradi huo ambao upo katika kipindi cha matazamia ya mwaka mmoja umetekelezwa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) na kusimamiwa na kampuni ya Doch.
Barabara hiyo ni kiungo muhimu kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na Mikoa ya Kaskazini pamoja na Kisiwa cha Ukerewe.
Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Mara katika ziara ya ukaguzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Sekta ya Ujenzi.
Post A Comment: