Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) Dkt. Jim Yonazi akisaini Rasimu ya Mkakati wa Kisekta wa kuratibu uwajibikaji wa mapambano dhidi ya kifua kikuu Nchini.

Na;Mwandishi wetu, Dodoma

Serikali imedhamiria kuendelea kushirikiana na wadau katika sekta zote ili kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) ifikapo mwaka 2030. 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi katika kikao na Makatibu Wakuu wa Wizara kilichofanyika katika ofisi za Waziri Mkuu Jijini Dodoma. 


“Ili kudhibiti ugonjwa huu wa Kifua Kikuu ni muhimu kushirikiana na wadau wengi kama sekta ya afya, wadau sekta ya elimu, sekta ya usafirishaji na sekta nyingine mbalimbali.” amesema Dkt. Yonazi.


Kwa upande wake Mtaalamu Mshauri kutoka Stop TB Partnership (STP) Bw. Oscar Mukasa wakati akiwasilisha taarifa ya mpango kazi wa kudhibiti Kifua Kikuu amesema watu wenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo ni pamoja na watu wanaoishi katika makazi duni, Watoto, Wavuvi na wanafunzi wanaoishi bweni.


 “Kuna makundi mengine ambayo yako hatarini kupata maambukizi Watu wenye VVU, watu wenye Utapiamlo, wachimbaji madini, wanaoishi na mgonjwa wa Kifua Kikuu, watoa huduma za afya na wanaotumia madawa ya kulevya kwa kujidunga sindano,” Ameeleza Mshauri huyo.


Aidha Bw. Mukasa amewashauri wanaoishi katika mazingira hayo kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB).




(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: