Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (wa pili kushoto) na viongozi mbalimbali wakivuta pazia kuashiria uzinduzi |
Na
Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amehimiza watumiaji wa maji kulipa ankara za maji kila mwezi bila kulaza ili kuiwezesha Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) iweze kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji, matengenezo na sehemu ya uwekezaji. Serukamba ameyasema hayo leo Machi, 17,2023 wakati akizindua mradi wa maji wa Kata ya Unyambwa uliogharimu zaidi ya Sh.Milioni 622 ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 6120. Serukamba alisema wananchi mbali na kulipa ankara za maji kwa wakati pia wajiepushe na vitendo vya wizi wa maji kwani jambo hilo linaongeza mzigo wa gharama kwa SUWASA na wateja wake. Aidha, Serukamba alitaja mambo mengine ambayo yataweza kuisaidia SUWASA kuwa ni kutunza vyanzo vya maji pamoja na miundombinu yote ya huduma, kutumia maji kwa uangalifu na kufuata taratibu zilizowekwa wakati wa kuomba maunganisho ya majisafi. Serukamba
alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa wananchi wa Kijiji cha Unyambwa na
uongozi wa kata hiyo hususani Diwani, Shabani Magwe kwa ushirikiano mkubwa
ambao wameipatia SUWASA katika hatua mbalimbali za ujenzi wa mradi huo ikiwemo
utoaji wa maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya maji na kuomba ushirikiano huo
uendelezwe hata wakati wa uendeshaji wa mradi kwa kuwa Unyambwa sasa ipo ndani
ya Manispaa na wananchi wanahitaji miundombinu ya majisafi iwekwe majumbani
mwao. Mkurugenzi
Mtendaji wa SUWASA, Sebastian Warioba alisema mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya
maji Kata ya Unyambwa, ni mradi wa awamu ya pili baada ya mradi wa awamu ya
kwanza kukamilika mwaka 2018. Alisema
mradi wa awamu ya kwanza ulihusisha uchimbaji wa kisima eneo la Unyambwa juu na
uligharimu kiasi cha Sh. Milioni 45. Warioba alisema mnamo mwaka 2019,
Watalaamu kutoka Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa kushirikiana
na watalaamu kutoka SUWASA walikamilisha taarifa ya usanifu wa mradi wa maji
katika Kata ya Unyambwa na taarifa iliwasilishwa Wizara ya Maji kwa maombi ya
fedha za utekelezaji wa mradi huo na kuwa Wizaraya Maji kupitia Mfuko wa Maji
(NWF) ilianza kutoa fedha za ujenzi wa mradi wa ujenzi miundombinu ya maji
Kijiji cha Unyambwa mwaka 2021. Aliongeza kuwa awamu ya pili ya mradi
wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika kata hiyo ulianza Juni 1,2021 na
ulitarajiwa kukamilika Septemba 01, 2021 na kueleza kuwa mradi huo haukukamilika
kwa tarehe iliyokuwa imepangwa kutokana na fedha za mfuko wa maji kutolewa kwa
awamu tofauti tofauti. Alisema mradi huo umetekelezwa kwa
kutumia watalaamu wa ndani wa SUWASA (SUWASA force account) na kuwa iwapo utekelezaji
wake ungetumia utaratibu wa mkandarasi gharama ingekuwa zaidi ya Sh. Milioni 869. Mwenyekiti
wa Bodi SUWASA, Deocres Kamala alisema mradi huo utawasaidia watu
katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazolenga kuleta maendeleo katika
Manispaa ya Singida, kama Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya maji mwaka huu
inavyosema 'Kuongeza Kasi ya Mabadiliko
Katika Sekta ya Maji kwa Maendeleo Endelevu ya Kiuchumi' na kuunga mkono
jitihada za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru alisema mradi huo unakwenda kuwaondolea adha waliokuwa wakiipata wajawazito wakati wa kwenda kujifungua kwenye Zahanati ya kata hiyo kwani walilazimika kwenda na vidumu vya maji. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi huo wa maji. |
Post A Comment: