Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange ameagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha kupeleka timu maalum katika jijiji la Arusha kufanya uchunguzi ili kujiridhisha na gharama zilizotumika katika miradi mitatu ambayo ilipelekewa fedha za ujenzi lakini fedha imeisha na miradi haijakamilika.
Ametoa maelekezo hayo leo tarehe 09 Machi 2023 wakati alipoambatana na Mbunge Jiji la Arusha, Mhe. Mrisho Gambo kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.
Miradi hiyo ni Ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa nje na Kliniki ya Mama na Mtoto katika Zahanati ya Olkereyan, ujenzi wa shule mpya kata ya Mriet pamoja na ukarabati wa majengo 6 kituo cha afya Mkonoo kata ya Terati.
Awali, Dkt. Dugange alikagua Ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa nje na Kliniki ya Mama na Mtoto katika Zahanati ya Olkereyan kata ya Moshono ambao umetumia shilingi milioni 100 lakini bado haujakamilika na unahitaji milioni 50 za ukamilishaji.
Ameelekeza Halmashauri kutotumia fedha ya ziada ya milioni 50 iliyopelekwa kukamilisha ujenzi hadi timu ya uchunguzi itakapojiridhisha na matumizi ya milioni 100 iliyotumika awali katika ujenzi.
Aidha, Dkt. Dugange ameelekeza timu ya hiyo kufanya uchunguzi wa gharama na thamani ya fedha katika ujenzi wa shule mpya kata ya Mriet ambayo inajengwa kwa muundo wa ghorofa.
Amesema timu hiyo ijiridhishe na ongezeko la gharama za mradi ambapo awali Serikali ilitoa Milioni 470 lakini kumekuwepo na ongezeko gharama za ujenzi hadi kufikia milioni 840 lakini ujenzi haujakamilika.
Kadhalika, Dkt. Dugange ameelekeza timu hiyo ifanye uchunguzi na kujiridhisha na matumizi ya milioni 800 iliyotolewa kujenga na kufanya ukarabati wa majengo 6 kituo cha afya Mkonoo kata ya Terati ambapo pesa imeisha na majengo hayajakamilika.
Ameeleza kuwa shilingi milioni 800 ilitakiwa kukamilisha miundombinu yote katika kituo cha Afya Mkonoo lakini bado inahitajika zaidi ya milioni 91 za kukamilisha jengo la upasuaji na Mama na Mtoto.
Dkt. Dugange amesema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi za maendeleo lakini watumishi wachache wanashindwa kutekeleza majukumu ya kusimamia fedha hizo kikamilifu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jiji la Arusha, Mhe. Mrisho Gambo ameeleza kuwa pesa zilizotumika katika mradi hiyo haziendani na kazi iliyotumika katika miradi hiyo.
Mhe. Gambo amesema miradi mingi inayoendelea kutekelezwa taratibu za manunuzi hazifuatwi ambapo wataalam waliopewa dhamana wanaenda kinyume na maelekezo na miongozo ya Serikali hali inayopelekea kuwepo kwa upotevu wa fedha wakati wa utekelezaji wa za miradi.
Post A Comment: