Ripoti mpya kuhusu pengo la usawa katika fursa ya kupata maji safi ya kunywa na masuala ya usafi na kujisafi inaonyesha kwamba zaidi ya nusu ya watu wote duniani hawana fursa ya kupata huduma salama za usafi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo kwa ushirikiano wa shirika la afya duniani WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, mabilioni ya watu duniani wanaendelea kutaabika kutokana na kukosa huduma bora za maji na masuala ya usafi.
Takribani watu bilioni 2.2 kote duniani, ripoti inasema hawana huduma ya maji salama ya kunywa, bilioni 4.2 wengine hawana huduma salama za usafi na watu bilioni 3 wanakosa huduma za msingi za shemu za kunawa mikoni.
Ripoti zinaonesha kwamba tangu mwanzo wa karne hii watu bilioni 1.8 wamepata fursa ya huduma za msingi za maji ya kunywa lakini hakuna usawa katika upatikanaji, uwepo na kiwango kinachohitajika cha huduma hizo.
Hali ipo tofauti katika Shule ya Sekondari Nanja Wilayani Monduli na vijiji vinavyozunguka shule hiyo ambapo wanafunzi wa shule hiyo wanaendelea kutaabika kwa kutumia maji ya kwenye mabwawa kwa ajili ya kufulia na kuogea.
John Haule ni mwanafunzi wa kidato cha nne anaeleza kuwa wamekuwa wakitaabika sana kupata maji ya kuogea na kufulia jambo ambalo linawafanya kwenda kuchota maji ya kwenye mabwawa kwa ajili shughuli hizo ingali maji hayo yanatumiwa na wanyama.
"Tunateseka sana kila siku jioni lazima tuvuke barabara kwenda kuchota maji wengine wanalazimika kuchota haya maji na kujimwagia na kufanya ndio wameoga tunaomba serikali kupitia wadhibiti ubora wa shule watuangalie kwa jicho la tatu"Alisema John
Wakati serikali ikiwa imetoa zaidi ya shilingi milioni 100 ya dharura kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji katika vijiji kadhaa wilayani Monduli Mkoani Arusha pesa hizo hadi sasa hazieleweki zimetumika katika mradi upi na kilio cha maji katika vijiji hivyo kuendelea kuwatesa wananchi na wanafunzi hadi sasa.
Octoba 20 mwaka jana Mamlaka ya Maji Mkoa wa Arusha {RUWASA} ilitoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa vijiji hivyo baada ya Mbunge wa Jimbo la Monduli,Fred Lowassa kuwasemea wananchi wake juu ya kukosekana kwa maji kwa jamii ya vijiji hivyo na serikali kusikia kilio chake.
Hata hivyo Diwani wa Kata ya Lepruko Yonas Masiaya alisema maji yaliyosambazwa katika vijiji 8 hayakuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wa vijiji hivyo hali iliyofanywa wananchi hao kuendelea kusaka maji usiku na mchana bila ya mafanikio.
Diwani alisema maji yaliyoletwa hadi katika vijiji hivyo hayafanani na fedha zilizotolewa na serikali na usambazaji wa maji katika maeneo ya huduma kama shule na afya bado watu walikuwa wakikosa maji kwani yaliyokuwa yakipelekwa kwa Bonza bado yalikuwa hayatoshi.
Miriam Mollel ni mkazi wa kijiji cha Nanja katika kata ya Lepruko anaeleza kuwa wamekuwa wakipata tabu sana kipindi hiki cha kiangazi kutokana na mabwawa kukauka maji na kusababisha wao kutembea umbali mrefu kufuata maji katika bwawa la nanja.
"Serikali iangalie namna bora ya kutusaidia sisi jamii ya wafugaji tunapata sana taabu kupata maji yaliyosafi na salama kwenye familia zetu,watoto wanakwenda shule bila kupata hata chai kutokana na kukosa maji" Aliongezea
Akizungumzia tukio hilo Meneja wa RUWASA Wilaya ya Monduli Nevile Msaki alishindwa kukanusha wala kuthibitisha utata wa shilingi milioni 100 na kusema kuwa hakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumza.
Mwishoni mwa mwaka jana 2022 mtandao huu ulifanikiwa kufika katika shule y asekondari nanja nakujiona hali mbaya waliyokuwa nayo wanafunzi wa shule hiyo wakitumia maji ya kwenye mabwawa kwa kuogea na kufulia jambo ambalo lilimuibua Mbunge wa Jimbo la Monduli na Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Arusha ambao walifanya ziara kwenye kijiji cha Mti Mmoja na kusema serikali imetenga milioni 100 za dharura kwa ajili yakupeleka maji kwenye Vijiji hivyo.
Post A Comment: