Mchungaji Yona Ezekiel wa Kanisa
la Moravian Parishi ya Sabasaba Singida

Na Dotto Mwaibale, Singida

WAZAZI na walezi wenye watoto walio katika makundi maalumu (walemavu) wametakiwa kutowafungia ndani badala yake wawapeleke shuleni na kwenye vyuo vya ufundi wakapate mafunzo ya fani mbalimbali.

Ombi hilo limetolewa na Mchungaji Yona Ezekiel wa Kanisa la Moravian Parishi ya Sabasaba,Machi 12, 2023 katika ibada iliyohudhuriwa na Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye Ulemavu Sabasaba kilichopo Manispaa ya Singida.

“Leo Mungu ametupa baraka kubwa ya kutembelewa na watoto wetu kutoka Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye Ulemavu Sabasaba na tumeona vipaji vyao vya uimbaji” alisema Ezekiel.

Ezekiel alisema wanafunzi hao wanafundishwa fani mbalimbali za ufundi kama umeme, uokaji wa keki, uchomeleaji, ufundi rangi, ushonaji, masuala ya saluni, uselemara, utengenezaji wa simu na upambaji.

Alisema wapo wanafunzi ambao wamefikia hadi masomo ya juu na kuwa wahandisi na wataalam katika maeneo mbalimbali hapa nchini hivyo wazazi wasiwanyime watoto wao fursa ya kupata mafunzo hayo yanayotolewa bure na Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alisema mtoto kuwa mlemavu hakumfanyi hashindwe kufanya chochote kwani kila mmoja anaweza kujifunza fani yoyote kulingana na ulemavu alionao na sio kuwatenga au kuwafungia ndani.

Mchungaji Ezekiel akihubiri neno la Mungu kutoka kitabu cha Yohana 4:27-42 akimuongelea mwanamke msamaria  katika kisima cha Yakobo wakati Yesu Kristo alipokuwa akitoka Uyahudi akielekea Galilaya kupitia Samaria alimshangaa mwanamke huyo akichota maji kisima cha mbali ili hali kulikuwa na visima jirani na eneo alilokuwa akitoka huko akichota maji hayo mchana badala ya asubuhi na jioni muda uliokuwa umezoeleka.

Baada ya mshangao huo Yesu alimuomba maji mwanamke huyo msamaria ambaye alimwambia Wayahudi na Wasamaria hawachangamani kwa lolote na inakuaje amuombe maji lakini Yesu alimjibu kuwa angemjua anayemuomba hayo maji angemuomba maji ya uzima.

Mwanamke huyo msamaria alimwambia Yesu kuwa hana chombo cha kuchotea maji wala hana kisima na isitoshe ni kirefu hivyo atapata wapi hayo maji ya uzima.

Yesu alimwambia kila atakayekunywa maji ya kisima cha Yakobo ataona kiu, lakini atakayekunywa maji atakayompa yeye hataona kiu milele ndipo mwanamke huyo msamaria alipoomba apewe maji hayo ya uzima.

Mchungaji Ezekiel alitolea mfano huo akilinganisha na maisha yetu ya leo ambayo yamejaa utengano, ukabila, hakuna umoja, upendo jambo linalosababisha maendeleo ya nchi na huduma za kiroho kurudi nyuma badala ya kusonga mbele na kukithiri kwa vitendo vya ukatili.

Mchungaji Ezekiel alitumia nafasi hiyo kuiomba jamii kuwa na upendo, kuacha ukabila, umajimbo na badala yake kujenga utaifa na umoja kwa ajili ya kuijenga nchi yetu ya Tanzania na kila mmoja kuabudu kwa imani na dini yake kwa utulivu na amani jambo litakalo mpendeza Mungu.

Aidha Mchungaji Ezekiel ameendelea kuwaomba wadau mbalimbali kusaidia ununuzi wa kiwanja cha kujenga Kanisa la Moravian Parish ya Sabasaba kwani hivi sasa wanafanya ibada zao katika kanisa la muda walilolijenga kwa kutumia miti na mabati.

Mchungaji Ezekiel aliomba kwa mtu yeyote, Taasisi, Wafanyabiashara na madhehebu mbalimbali watakao kuwa tayari wanaweza kutoa kiasi chochote cha fedha kupitia Akaunti  Namba 50810046663 Benki ya NMB Kanisa la Moravian Sabasaba Singida mjini au awasiliane na Mchungaji Yona Ezekiel kwa namba 0758148508.


Mchungaji Yona Ezekiel wa Kanisa la Moravian Parishi ya Sabasaba, akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye Ulemavu Sabasaba Singida baada ya ibada iliyofanyika kanisani hapo leo Machi 12,2023.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: