Mchimbaji mdogo wa madini, Richard Lyamuya, mkazi wa Manispaa ya Singida, akizungumza na waandishi wa habari leo (Machi 21,2023) kuhusu madai ya Ofisi ya Madini Mkoa wa Singida kukataa kumpatia leseni ya uchimbaji wa madini.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MCHIMBAJI mdogo wa madini, Richard Lyamuya, mkazi wa Manispaa ya Singida ,
amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati apate haki yake baada ya
Ofisi ya Madini Mkoa wa Singida kukataa kumpatia leseni wakati amefuata
taratibu zote kwa kulipia ada tatu zilizoainishwa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (Machi 21,2023) amesema alipeleka
maombi ya kupatiwa leseni ya uchimbaji dhahabu katika kijiji Cha Matongo
wilayani Ikungi ambapo ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida ilimwelekeza
alipie ada ya maombi,ada ya maandalizi na ada ya pango na vyote alilipia kama
kawaida na kupewa stakabadhi.
Lyamuya alisema katika hali ya kushangaza baada ya leseni kutoka ili
akabidhiwa Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Singida, Chone Malembo, amekataa kusaini
leseni iweze kutoka kwa madai eneo aliloomba lina mgogoro jambo ambapo limezua
maswali yasiyo na majibu kwasababu kama ofisi hiyo ilijua eneo hilo lina
mgogoro ni kwanini ilimruhusu kulipia ada hizo.
Alisema amefuatilia suala hilo kwa kuandika barua katika ofisi ya Madini
Mkoa wa Singida,Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi na kwa Mkuu wa Mkoa lakini
bahati mbaya hajapata msaada wowote.
'Katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi nimefika zaidi ya mara saba bahati mbaya sikufanikiwa kuonana na Mkuu wa Wilaya badala yake nilionana na Afisa Tawala ambaye alinisikiza na akanipa majibu kuwa ameongea na Afisa Madini wa Mkoa wa Singida akasema leseni ninayoilalamikia hataweza kunipa bali niendelee na leseni nyingine nilizonazo," alisema Lyamuya.
Aliongeza jambo la kushangaza wakati tayari ameshafanyiwa mchakato na
kusubiri kupata leseni baadhi ya maofisa katika ofisi ya Madini Mkoa wa
Singida waliweka ombi namba PML145961/CZ Septemba 3 mwaka jana kwenye mtandao
katika eneo hilo hilo ambalo yeye ameomba leseni lakini baadaye ombili hilo liliondolewa..
Lyamuya alisema baada ya kufika katika ofisi zote za serikali bila
mafanikio Machi 13, mwaka huu mwanasheria wake wa kampuni ya Kim & Co
Advocates aliiandikia barua ofisi ya Madini Mkazi Mkoa wa Singida kutaka mteja
wao apewe leseni yake kwa kuwa amefuata taratibu zote.
"Unachokifanya sio matakwa ya sheria bali ni utashi wako kama mtu binafsi,hakuna
mgogoro wa kiuchimbaji katika leseni hii na hata mgogoro ungekuwepo basi
kifungu cha 102 cha sheria ya Madini namba 14 ya 2010 kingetumika na kwa niaba
ya Kamishina wa Madini ungeendesha nafasi hii ya kimahakama na kutoa maamuzi
ya mgogoro lakini tunachokiona unashughulika na upande mmoja wa mteja
wetu," imeeleza sehemu ya barua hiyo ambayo ameandikiwa Afisa Madini Mkoa
wa Singida.
Mwanasheria wa mchimbaji huyo Raymond Kim, amendelea kueleza katika barua
yake hiyo kwa kutoa angalizo kwamba mteja
wao atawajibika kuchukua hatua za kisheria kama ofisi ya Madini Mkoa wa Singida
itaendelea kukataa kutoa leseni namba PML 0734SGD ambayo leseni hiyo ilitokana na ombi namba PML 133372/CZ.
"Hatua itakayofuata ni kufungua kesi mahakamani dhidi yako wewe
binafsi na kuwajibika kulipia fidia zote za kisheria ikiwa ni pamoja na hasara
na gharama za kesi," imeeleza barua hiyo kwenda kwa Afisa Madini Mkoa wa
Singida.
Kufuatia hali hiyo,amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati suala
hilo kwakuwa amefuatilia katika ofisi nyingi za serikali na hajapata msaada.
Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Singida, Chone Malembo, alipoulizwa alikiri
kuufahamu mgogoro huo na kuwa ulianza baada ya watu wawili kujitokesa kwamba
eneo hilo aliloomba leseni Lyamuya (mchimbaji) ni shamba lao.
Alisema walibaini eneo
aliloomba Lyamuya lina mgogoro wakati tayari ameshafanya mchakato wa
malipo na alipoulizwa na waandishi kama je fedha hizo atarudishiwa mchimbaji
huyo alijibu hilo ni suala jingine bila ya kufafanua zaidi.
Malembo alisema ofisi yake itaendelea kufanya mchakato wa kusuluhisha kati ya wenye shamba ambao nao wanataka wafanye uchimbaji kwenye eneo hilo kama wataona inafaa wafanye ubia wa uchimbaji.
Mkaguzi Mkuu wa mgodi huo, Japhet Madusa akizungumzia changamoto iliyojitokeza katika eneo hilo. alisema katika migodi mbalimbali ambayo amewahi kufanya kazi mmiliki wa shamba amekuwa akipewa asilimia 10 hadi 20 na mwekezaji mwenye leseni lakini imekuwa tofauti katika mgodi huo ambapo mwenye shamba anataka apewe mgao sawa na mwekezaji jambo ambalo linaleta changamoto.
Mkaguzi Mkuu wa mgodi huo, Japhet Madusa akizungumzia changamoto iliyojitokeza katika eneo hilo.
Muonekano wa maeneo kadhaa ya mgodi huo.
Taswira ya mgodi huo.
Muonekano wa mgodi huo.
Post A Comment: