Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira zinafanyiwa tathmini ili kuongeza kasi zaidi katika utekelezaji wa miradi ya maji, pia kutambua mchango wa watendaji katika taasisi hizo.
Dkt. Mpango amesema hayo wakati akizindua Ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ya mwaka 2021-2022 wakati wa Wiki ya Maji jijini Dar es salaam ambapo amesisitiza kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maji, hivyo juhudi na kujitoa katika kazi ni muhimu ili wananchi wapate maji kama ilivyopangwa na Serikali.
“Mamlaka za Maji ziendeshwe kibiashara, tusipoteze hela, tubadilike na kuboresha huduma” Dkt. Mpango amesema na kusisitiza kuwa baadhi ya watumishi wa mamlaka za maji wanatuhumiwa kushirikiana na vishoka katika kufanya hujuma mbalimbali katika kutoa huduma za majisafi.
Pamoja na hilo amezitaka mamlaka za maji kuhakikisha zinahakiki ubora wa maji yanayozalishwa kabla ya kumfikia mteja.
Dkt. Mpango ameiagiza Wizara ya Maji kuorodhesha taasisi zote za umma zilizolimbikiza madeni ya huduma ya maji na kuelekeza ziwe zimelipa madeni hayo ifikapo robo ya kwanza ya mwaka 2023-2024. Pamoja na hilo, ameelekeza kupatiwa taarifa ya miradi ya maji iliyochukua muda mrefu katika utekelezaji wake, miradi iliyochukua muda wa zaidi ya miaka mitano.
Amesema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa kikwazo katika kupata maji kwa sababu ya uharibifu wa mazingira hivyo mamlaka za maji na bodi za maji za mabonde wafanye tathmini ya vyanzo vya maji vyenye uhakika, na kushirikiana katika kutekeleza sheria inayohusu uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Dkt. Mpango ameainisha kuwa kiwango cha upatikanaji maji kimeongeza kutoka asilimia 70.1 hadi 77 kwa vijijini na mjini kutoka asilimia 84 hadi 88, na lengo hasa ni kufika asilimia 85 vijijini na 95 mjini.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema EWURA imetoa mchango mkubwa katika mafanikio ya sekta ya maji katika kuwafikishia wananchi huduma toshelevu ya maji.
Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Cyprian Luhemeja akiongea awali amesema hivi sasa vijiji 9,144 vinapata huduma ya maji, na mpango ni kufika katika vijiji 12,319 ili kuimarisha huduma ya majisafi jumla ya miradi 996 inaendelea kutekelezwa nchini.
Katika utoaji tuzo, mamlaka za Dakawa, Vwawa-Mlowo na Makonde zimeonekana kuwa zinahitaji maboresho zaidi hivyo kutakiwa kuonana na Makamu wa Rais Dkt. Mpango kabla ya kuondoka eneo la tukio.
Mamlaka zilizofanya vizuri na kuwakilisha nyingine katika tuzo ni, katika kuwasilisha tozo za udhibiti ni mamlaka za Lushoto na DAWASA; Udhibiti wa upotevu wa maji mamlaka za Maganzo, Shinyanga na KASHWASA.
Nyingine zilizofanya vizuri na kuibuka kinara katika kufikia malengo ya kibiashara ni mamlaka za Orkesumet, KASHWASA na DUWASA. Eneo la huduma ya majisafi na usafi wa mazingira ni mamlaka za Biharamulo, Arusha,Moshi na Igunga.
Vinara wa kutoa huduma ya majisafi na mazingira ni mamlaka za Nzega, KASHWASA (miradi ya kitaifa) na Iringa.
Katika hafla hiyo mamlaka 38 kati ya 90 zimepewa tuzo baada ya kufanyiwa tathmini katika Ripoti ya 14 ya EWURA.
Post A Comment: