Kundi la Machinga Mkoa wa Dodoma wamefanya maandamano ya amani ya kumpongeza Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaheshimisha ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.
Akipokea maandamano hayo ya amani Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewapongeza wafanyabiashara wadogowadogo (Machinga) kwa kufanya kazi zao kwa utulivu na juhudi na kutambua mchango wa Rais Mama Samia Suluhu katika kipindi cha miaka miwili madarakani.
"Ninayo furaha kwasababu kundi hili ambalo nchi yetu imekuwa ikihangaika nalo leo ni kundi ambalo linafuraha na amani na linafanya kazi zake kwa utulivu katika mkoa wetu niwapongeze kwa juhudi, Utashi, busara na hekima na ndio maana leo hii mmeona umuhimu wa kumpongeza Mhe. Rais wetu.
"Jambo mlilofanya Leo linaipa fahari Dodoma kama ambavyo risala yenu inasema Mambo yaliyofanyika ni mengi mno na yataandikwa kwenye historia ya nchi ya Tanzania lakini huenda Afrika Mashariki kwasababu Machinga Dodoma ni sehemu ya mfano na nyie mmewaona wageni mbalimbali wakitembelea hapa kufanya utalii."Amesema Senyamule
Kwa upande wake Mwenyekiti Msaidizi Machinga Mkoa wa Dodoma Bw. Christian Msumari ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuwatambua kama kundi rasmi na kuwaweka chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu jambo ambalo linawapa urahisi wa kutimiza majukumu yao kwa kusimamiwa na kupatiwa Mafunzo mbalimbali.
"Tunashukuru kwa kututambua kama kundi rasmi na kutuweka chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu na kwa kufanya hivo imetumefanya tuweze kupata Mafunzo ya uongozi na tumepata Wizara ya kutulea na kutusaidia.
"Tunamshukuru mama kwa kutupatia mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji inayolenga makundi ya vijana, wanawake, walemavu na Machinga tukiwa kundi jipya lililoongezwa kunufaika na mikopo na sisi tumenufaika nayo kupitia vikundi vya watu watano na kila aliyekidhi vigezo amepatiwa shillingi milioni 1" Amesema Bw. Msumari
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri amewaasa wamachinga wa soko hilo kutunza miundombinu ya soko hilo ili kuendelea kufanya kazi zao kwa urahihisi na kuhakikisha linadumu kwa muda mrefu.
Hafla hiyo imeadhimishwa kwa kaulimbiu ya "miwili ya mama fur-SAMIA kwa wamachinga" huku mgeni rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule, halfa iliyofanyika katika soko la Machinga Complex Dodoma na kuandaliwa na wafanyabiashara wenyewe.
Post A Comment: