Na John Walter-Manyara
Hospitali ya Lutheran Haydom jimbo la Mbulu kwa kushirikiana na Wizara ya afya na chama cha Madaktari (TAMA) wamefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama na watoto kwa asilimia 50% kupitia mradi wa kitita cha uzazi salama (Safe births Bundle of care).
Watoto wachanga chini ya siku moja ambao walikuwa wafe, wameokolewa na watoto wanaozaliwa wafu (Still birth) wamepungua kwa Zaidi ya asilimia 25 kwenye vituo vyote ambavyo mradi unatekelezwa, huku vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutokana na kuvuja damu nyingi vikipungua kwa zaidi ya asilimia 10%.
Mradi huo wa miaka mitatu unaolenga kuokoa maisha ya Mama na mtoto wakati na baada ya kujifungua (Saving Mothers and Babies During and after Birth), unafadhiliwa na kitengo cha benki ya dunia (Global Financing Facility) ambapo baada ya kupokea andiko kutoka Hospitali ya Haydom, benki ya dunia imetoa Dola Milioni 4.5 Zaidi ya shilingi bilioni 10.5 za kitanzania.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Kilutheri Haydom Dr. Pascal Mdoe amesema mradi unatekelezwa katika vituo 30 kwenye mikoa mitano ya Manyara, Mwanza, Shinyanga, Tabora na Geita ambapo kila mkoa una vituo sita.
Amesema vituo hivyo vilichaguliwa na serikali kwa kuzingatia idadi ya vifo vya akina mama na Watoto haswa wakati wa kujifungua.
Aidha Mradi huo ulianza kutekelezwa Novemba mwaka 2020 kwa kufanyika utafiti na unatarajiwa kukamilika Novemba 2023.
Naibu waziri wa afya Tanzania Dr.Godwin Mollel, amesema mradi huo ni muendelezo wa dhamira ya serikali ya rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha Afya ya mama na mtoto.
Amesema kwenye Hospitali za mikoa nchi nzima serikali imepeleka Zaidi ya shilingi billion 54.2 huku shilingi 51.2 zikipelekwa katika hospitali za kanda na taifa.
Amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani kulikuwa na CT Scan mbili pekee ambapo hadi kufikia sasa ameweka CT Scan katika hospitali zote nchini.
Kwenye eneo la vifaa tiba kwa hospitali za mikoa, kanda na Taifa serikali imewekeza zaidi ya Shilingi billioni 290.9 kwa mwaka 2023.
Dr. Mollel amesema kwa hospitali za taifa hadi za wilaya zimejengwa ICU ambazo zinasaidia kuokoa maisha ya akina mama na watoto, ujenzi uliogharimu shilingi billioni 24.8 na vifaa vimegharimu billion 61.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa maendeleo wa Norway Bjorg Sandkjaer amefurahishwa sana na mpango huo na kwamba nchi mbili wataendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuwa viongozi na wananchi wana umoja.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu Kheri James amesema dhamira ya serikali kupitia mipango yake na washirika wa maendeleo wameendelea kusimamia mkakati wa pamoja wa kuhakikisha wanaokoa maisha ya mama na mtoto.
Post A Comment: