Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, tarehe 15 Machi, 2023 wametembelea wilaya ya Korogwe ili kukagua na kujionea utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kupongeza kwa namna nishati ya umeme, inavyobadilisha maisha ya Wananchi wengi wa vijijini.

Wajumbe wa Kamati hiyo; waliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dunstan Kitandula na Makamu Mwenyekiti Mhe. Judith Kapinga walianza ziara yako wilayani Korogwe kwa kutembela kijiji cha Mswaha Darajani katika Halmashauri ya wilaya ya Korogwe vijijini ambapo walijionea kaya zilizonufaika kwa kuunganishwa na umeme kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini wa REA Awamu ya Tatu (Mzunguko wa Pili) ambapo zaidi ya kaya 20 zimeunganishwa na nishati ya umeme.

Pamoja na kutembea kijiji hicho; Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge pia walishiriki kwenye mkutano wa hadhara ili kusikiliza changamoto zinazowakabili Wananchi; ambapo wengi wameonekana kuhitaji nishati ya umeme kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Dotto Ally, mkazi wa kijiji cha Mswaha Darajani ametoa ombi kwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa kipaumbela kwa Wananchi wa eneo hilo kwa kuwa Watu wengi wanahitaji nishati ya umeme na kwamba wapo tayari kuunganisha (Wiring) na kutumia nishati hiyo.

“Sisi upande wa juu wa kijiji tunahitaji sana umeme na tunaomba tufikiriwe, ukilinganisha na wananchi wa upande wa chini”. Alisema Bwana Dotto.

Katika hatua nyengine, Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini; wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Dunstani Kitandula na Mhe. Tabasamu Mwagao walishiriki katika tukio la kuwasha umeme katika shule ya msingi Mswaha pamoja na msikiti wa Mswaha Darajani (Al Massijid Munauwara) katika kata ya Mswaha, kuashiria kuanza rasmi kutumika kwa nishati ya umeme katika eneo hilo.

Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la uwashaji wa umeme katika shule hiyo na msikiti; Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini walielekea katika kata ya Madumu, kitongoji cha Chekelei, Halmashauri ya wilaya ya Korogwe vijijini kwa ajili ya kuzungumza na Wanafunzi wa shule ya sekondari Chekelei na Wananchi wa eneo hilo.

Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato aliwaeleza Wananchi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, imetoa kipaumbele ili kuhakikisha Wananchi wa vijijini, wanapata nishati ya uhakika na kuwataka kuwa wavumilivu kwa kuwa miradi ya nishati ya uhakika inahitaji uwekuezaji mkubwa na endelevu na kwamba mambo yote, yanatekelezwa kwa awamu.

“Nataka niwahakikishie kuwa kazi ya kuleta nishati ya umeme na nishati nyengine, ni endelevu, tuwe wavumilivu”. Alisisitiza Naibu Waziri Byabato.

Aidha; Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mhe. Philipo Mulugo waliwasha taa katika darasa katika shule ya sekondari ya Chekelei ili kuashiria kuanza rasmi kutumia kwa nishati ya umeme katika shule hiyo.

Akiongea na niaba ya Wabunge wenzake; Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Kirumbe Ng’enda ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita; inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea Wananchi maendeleo kupitia nishati mbalimbali.

“Nitoe wito kwa Wananchi kuendelea kuilinda miundombinu ya umeme, Serikali inatumia gharama kubwa kuianzisha na kuiendeleza, ninyi Korogwe mna bahati ya kupata fursa ya umeme, kuna maeneo kule Kigoma, ninapotoa, hawajafikiwa na fursa kama hii, mliyonayo”. Alisisitiza Mbunge huyo wa Kigoma Mjini.

Naye Meneja wa Usimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena amesema, Serikali imetoa bilioni 25 kwa ajili ya kugharamia miradi ya kupeleka nishati ya umeme katika Halmashauri ya wilaya ya Korogwe vijini, Mkinga na Pangani na kuongeza kuwa fedha zipo ili kuhakikisha Wananchi wengine wanaendelea kufikiwa na nishati ya umeme.









 

 

Share To:

Post A Comment: