Kamati ya kudumu ya Bunge, Elimu Utamaduni na Michezo leo imetembelea na kukagua utekelezaji wa Miradi mbalimbali inayotekelezwa na Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya Kivukoni ambapo pamoja na mambo mengine kamati imekipongeza Chuo kwa kuendelea kutekeleza Miradi ya Maendeelo pamoja na kutoa Kozi ya Uongozi, Utaifa na Maadili.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Wabunge wa kamati hiyo huku wakikitaka Chuo kuendelea kudumisha na kuenzi falsasa za baba wa Taifa kwa lengo la kutimiza malengo na dhamira inayokusudiwa.
“Nakipongeza sana Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere niseme tu sisi Wabunge tutaenda kushauri serikali kwa lengo la kuongeza fedha ili kukamilisha Miradi inayotekelezwa na Chuo hiki, hongereni pia kwa kuanza kutekeleza miradi kwa kutumia makusanyo ya ndani,” alisisitiza Mheshimiwa Esther Maleko.
Wabunge hao pia wameutaka uongozi wa Chuo kupeleka mafunzo ya Uongozi, Utaifa na Maadili Kwenye ngazi za Chini hadi ngazi ya Kitaifa ili kuhakikisha Taifa linakuwa na vijana ambao ni wazalendo na wenye maadili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo Profesa Kitila Mkumbo amesisitiza suala la miradi kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano ya Mikataba, huku akisisitiza kukamilishwa kwa Miradi inayotekelezwa visiwani Unguja na Pemba.
Profesa Mkumbo ameainisha suala la kuboresha bunifu mbalimbali ambazo zinabuniwa Chuoni ikiwa ni pamoja na kuziendeleza ili ziweze kusaidia na kutatua changamoto zinazoikali Jamii.
Aidha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda amesema Chuo kina bunifu nyingi ambazo zipo katika hatua kadhaa changamoto ni kukubalika na kuingia sokoni.
Naye Mkuu wa Chuo Profesa Shadrack Mwakalila amewaeleza Wabunge hao kuwa ujenzi wa Maktaba katika Kampasi ya Kivukoni utawezesha Wanafunzi 2500 kujisomea kwa mara moja, lakini pia kutakuwa na kumbi za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi 1000.
Profesa Mwakalila alibainisha Changamoto kuu katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kuwa ni ufinyu wa bajeti na kuiomba Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuishauri Serikali kuongeza fedha kukamilisha miradi inayoteklezwa na Chuo chicho.
Hata hivyo Meneja anayesimamia mradi huo kutoka vikosi vya ujenzi Mhaandisi Mwesigwa Ichwekeleza amesema mpaka sasa kiasi cha Shilingi Bilioni mbili nukta saba zimeshalipwa na mradi umefikia asilimia 30 na mradi huo untarajia kukamilika mwaka 2024.
Imetolewa na:
KITENGO CHA HABARI NA MASOKO
CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE
16.03.2023
Post A Comment: