Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Japhet Hasunga, akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa kiwanda cha mipira ya mikono cha Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Idofi-Makambako mkoani Njombe.
Na Mwandishi Wetu, Njombe
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema imeridhishwa
na maendeleo ya mradi wa kiwanda cha mipira ya mikono cha Bohari ya Dawa (MSD)
kilichopo Idofi-Makambako mkoani Njombe na kuahidi kuishauri serikali kuongeza
bajeti ya shilingi bilioni 12, kuwezesha mradi huo kukamiloka kuanza kazi
ifikapo Julai mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Japhet Hasunga, amesema kamati
imeishauri bodi ya Wadhamini MSD na Menejimenti kuwa wabunifu kufikia adhma ya
serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kufikia
uchumi wa viwanda.
Amesema kutokana na tathimini ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
inaonyesha ujenzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 70, ambapo kamati imeona
haja kwa hatua zilizobaki taasisi za udhibiti kuhakikisha zinashirikiana
ipasavyo kuwezesha bidhaa zitakazozalishwa kukidhi viwango vya kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Rosemary Silaa, ameeleza kuwa
kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha asilimia 83 ya mahitaji ya mipira
ya mikono nchini, ambapo, bodi itahakikisha inaisimamia ipasavyo MSD kufuata
kanuni, taratibu na sheria.
Amesema wapo kwenye hatua za kutekeleza mkakati wa kampuni tanzu
itakayosimamia shughuli nzima za uzalishaji na MSD kubaki na wajibu wake wa
kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, aliwasilisha kwa kamati hiyo taarifa ya mradi na kuomba ongezeko la fedha ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji ipasavyo mwezi Julai mwaka huu na kuwaomba wajumbe hao wa Kamati ya PAC kuwa mabalozi wa mradi huo
Post A Comment: