Na;Elizabeth Paulo, Dodoma


Watanzania wametakiwa kujiwekea malengo ya kuweka akiba kidogo kidogo kwa ajili ya kwenda kutembelea hifadhi za wanyama pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.


Pamoja na wito huo kadhalika wawekezaji wameshauriwa kuwekeza kwenye mashamba ya zabibu kwa kujenga hoteli za kisasa na nyumba za kulala wageni ili kuwavutia watu kwenda kuona mashamba hayo na kupata mvinyo ikiwa ni kufanya utalii wa ndani.


Kamishna Msaidizi Mwandamizi Jeshi la Uhifadhi Ofisi ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kiunganishi cha hifadhi hiyo Dodoma Dkt. Noelia Myonga amesema wanaendelea kutoa elimu kuhamasisha jamii kufahamu utalii wa ndani.


Dkt.Myonga ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kutoa ufafanuzi kuhusiana na TANAPA na namna gani waandishi wanaweza kutumia kalamu zao vizuri ili kuelimisha jamii juu ya sekta nzima ya utalii.


 "Tujitahidi sana kwenye kalamu zetu kuandika habari zinazotuletea tija na Mungu atawabariki mkitumia kalamu zenu vizuri kwa kuandika ukweli na sio kupotosha kwani mkipata elimu nyie na wanachi wataelimika kupitia nyie kama kioo cha jamii".Alisema Dkt. Myonga



Aidha amesema kuwa malengo yao kama TANAPA ni hadi kufikia mwaka 2025 Tanzania iwe imeshatembelewa na watalii milioni tano(5) ikiwa pia ni lengo la serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt.Samia Suluh Hassan ambaye amefungua njia kwa watalii kuja Tanzania na kuonyesha nia ya dhati na sekta hii ya utalii.


 "Tunatoa elimu ya uhifadhi na kutoa elimu ya kuhamasisha utalii wa ndani kwa jamii kila mtu kwa nafasi yake anatakiwa avisemee vivutio vyetu ili wananchi waweze kuvijua kwa maana ya watalii wa ndani na watalii wa nje"Amesema Dkt.Noelia


 Pamoja na hayo amesema kazi yao ni kuhifadhi rasilimali zote zilizopo chini ya TANAPA huku TFS wenyewe wamejikita kwenye mambo ya misitu ambapo kuna sheria inayotofautisha mamlaka hizo na nyingine lakini hawa wote TAWA na TFS wanafanya kazi kwa ukaribu,kushirikiana pamoja na kushauriana. 


" Niwapongeze waandishi wa habari kwa kuweza kujitoa kufanya habari za utalii,kutangaza vivutio vyetu tena kwa kuamua kujilipia wenyewe kwenda kujionea vivutio vyetu jambo ambalo halijawahi kutokea nawapongeza sana". Aliwapongeza Wanahabari


Amesema,ni muda mrefu sasa kumekuwa na harakati mbalimbali za kuhamasisha utalii kwa watu wanaojiweza na kusema kuwa sasa ni zamu ya kuangalia makundi maalumu na kuwapa haki sawa jambo ambalo linaenda sambamba na matakwa ya haki za binadamu. 



"Serikali yetu inazingatia haki,na hakuna ubaguzi na sisi kama TANAPA tukiwa na dhamana ya hifadhi rasilimali nyingi za utalii tunataka kuanza kuyakumbuka makundi haya ,tuna Imani kupitia kwao jamii itaelewa umuhimu wa utalii"

Dkt.Myonga ameyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na wazee, wasiojiweza,watu wenye ulemavu mbalimbali ikiwemo Viziwi,walemavu wa viungo na wengine.


Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa TANAPA Dodoma Frederick Malisa ameeleza juhudi zinazofanywa na Ofisi hiyo kuwa ni kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani kwa kutoa elimu ya utalii hali itakayosaidia kuondoa taarifa zisizo sahihi zinazohusu utalii kwa wananchi.


Amesema jamii inapaswa kuelewa kuwa kila hifadhi ina kionjo chake hivyo kuwataka watanzania kwa ujumla kusherehekea mema ya nchi

yao kwa kupanga muda kutembeleahifadhi zote 22 ikiwemo Kigosi,Kisiwa cha Saanane,Kitulo, mto Ugala na Ibanda-Kyerwa.


Akitolea mfano wa hifadhi ya Burigi-Chato, Mhifadhi huyo amesema ni ya kujivunia kwa kuwa ina maziwa makubwa matano yenye mvuto duniani ikiwemo Burigi yenyewe na kutumia nafasi hiyo kuwashauri wadau wote wa maendeleo kuona haja ya kutembelea hifadhi zote kila mara.


Kutokana na hayo,baadhi ya wanahabari hao wa Utalii wameeleza kuwa wametia nia kutumia kalamu zao kuhamasisha jamii kufanya utalii wa ndani ili kutangaza vivutito nakukuza Uchumi huku wakisema ni wakati ambapo dunia inapaswa kujua vivutio vilivyopo nchini hali itajayohamasisha watalii wengi zaidi kufika Tanzania na kuongeza mapato kwenye sekta ya utalii.


Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: