Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na kuzifanyia tathimini nchi mbalimbali ili kujua uwezo wake wa kukopesheka katika masoko ya fedha ya Kimataifa, Moody’s, imetua nchini kwa ajili ya kufanya tathimini hiyo Tanzania.

 

Akizungumza wakati akiikaribisha timu ya wataalam kutoka Taasisi hiyo Jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema kuwa tathimini hiyo ni fursa kwa Tanzania kuweza kuyafikia Masoko ya fedha ya Kimataifa yatakayoiwezesha nchi kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.

 

Amesema kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika licha ya changamoto za Uviko 19 na Vita vya Ukraine na Urusi lakini pia Taifa limepiga hatua kubwa za kiuchumi, kidiplomasia, haki za binadamu na kisiasa.

 

Dkt. Mchemba alisema kuwa tathimini huru inayofanywa na Taasisi hiyo maarufu Duniani ya Moody’s inaiwezesha Tanzania kuaminiwa na Taasisi za fedha za kimataifa hivyo kuchochea uwekezaji ambao utakuza uchumi wa nchi pamoja na ajira kwa vijana.

 

Alisema kuwa ujio wa wataalam hao unajibu kiu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyeagiza nchi ifanyiwe tathimini ili kubaini uwezo wake wa kuyafikia masoko ya fedha ya kimataifa katika kuharakisha maendeleo ya watu.

 

Moody’s inaifanyia tathmini Tanzania kwa njia shirikishi itakayowezesha kutoa taswira halisi ya nchi na hatua ambazo imepiga kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Share To:

Post A Comment: