Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo wa kwanza kulia akitembelea shule ya msingi Majogo kujionea hali halisi ya Madarasa ya shule hiyo yalivyochakaa
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo akiwa na viongozi mbalimbali wametoka kujionea hali halisi ya Madarasa ya shule ya msingi Majogo yalivyo


Na Fredy Mgunda, Nachingwea.


MKUU wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo ameamuru kuvunjwa kwa baadhi ya Madarasa ya shule ya msingi Majogo katika Kijiji cha Litula kata ya Marambo kutokana na uchakavu wa majengo ya shule hiyo ambayo yanahatarisha maisha ya wanafunzi na walimu.

Akiwa katika ziara ya kijiji kwa kijiji yenye kauli mbiu isemayo "ulipo nipo toa kero yako sema kweli sio majungu",mkuu wa wilaya huyo alifanikiwa kufika katika shule ya msingi Majogo na kuikuta shule hiyo ikiwa katika hali ya uchakavu mkubwa wa majengo ambayo yanahatarisha maisha ya wanafunzi.

Moyo alisema kuwa haiwezekani wanafunzi wakaendelea kusoma kwenye madarasa ambayo yamejawa na nyufa kila kona hivyo madarasa hayo yabomorewe haraka iwezekanavyo.

Alimtaka mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea kujenga upya madarasa hayo ili wanafunzi wa Kijiji cha Majogo waendelee kupata elimu inavyotakiwa kwa faida ya Taifa.

"Uchakavu mkubwa wa miundombini,kuhatarisha maisha ya wanafunzi na walimu, siwezi kukubali hali ya shule ya msingi Majogo waendelee kusoma katika shule yenye majengo hatarishi"alisema Moyo

Moyo pia alimuagiza mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea kumalizia ujenzi wa vyoo vya shule ya msingi Majogo ili kuwalinda wanafunzi na walimu kiafya.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi walisema jengo la shule litaua wanafunzi,waomba libomolewe haraka haraka kwa kuwa wameshajenga jengo jipya la vyumba vya madarasa lakini havijamalizika.

Akijibu hoja hizo mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Injinia Chionda Kawawa alisema kuwa wameshatenga kiasi cha shilingi millioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa matundu mapya ya vyoo na wamelichukua suala la  kumalizia ujenzi wa vyoo ya shule ya msingi Majogo.

Kawawa alisema kuwa suala la umaliziaji wa jengo la shule ya msingi Majogo wamelichukua na watalifanyia kazi haraka sana ili kunusuru maisha ya wanafunzi na walimu wa shule hiyo.

Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: