Na John Mapepele
Serikali ya China na Tanzania zimetiliana saini mkataba wa Dola za kimarekani milioni moja kusaidia shughuli mbalimbali za kuendeleza Utalii kwenye Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
Mkataba huo umesainiwa leo Machi 16, 2023 kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro yaliyofanyika kwenye Ofisi za Makao makuu ya Hifadhi ya Kilimanjaro.
Wakati wa utiaji saini mkataba huo Tanzania imewakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Anderson Mutatembwa na Balozi wa China Mhe. Cheng Mingjian nchini ameiwakilisha nchi yake
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye ndiye Mgeni Rasmi ameshuhudia tukio huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua Tanzania duniani kupitia Mlima Kilimanjaro katika Filamu ya Royal Tour
Aidha, amesema Mlima Kilimanjaro unaopatikana nchini Tanzania ni nembo ya Afrika, kwani ndio mlima mrefu kuliko yote Afrika na kwamba Mlima huu pia ni mlima mkubwa duniani ambao upo huru kwa maana ya kwamba umesimama peke yake pasipo kuwepo kwa safu za milima kama ilivyo milima mingine duniani.
Ameeleza sofa nyingine za Mlima huo kuwa ni kuwa umeundwa na Kilele cha Kibo, chenye urefu wa mita 5895 (futi 19340), ambacho ndicho kivutio kikubwa kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi kwa sababu ya kufunikwa na theluji mwaka mzima.
"Lakini pia kuna vilele vingine kama Shira upande wa magharibi kikiwa na urefu wa mita 3962, na Mawenzi upande wa mashariki chenye urefu wa mita 5149. Kutokana na sifa hizi lukuki, hifadhi hii ilipewa hadhi ya kuwa urithi wa dunia mwaka 1987 iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). " Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Pia amesema Mlima Kilimanjaro umeendelea kuwa kivutio kikubwa cha watalii wanaotembelea hifadhi hii, hivyo kutoa ajira kwa jamii jirani na Taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa Mlima huo ni chanzo kikubwa cha maji yanayotumika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa jirani. Maji haya hutumika majumbani, umwagiliaji, viwandani na uzalishaji wa umeme.
Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo kwa Shirika la Hifadhi la la Taifa Tanzania (TANAPA) na Wizara yake kuendelea kuboresha miundombinu na usalama kwa wageni
Katika tukio hilo Mhe. Mchengerwa pia ametoa tuzo kwa watu mbalimbali wanamchango kwenye Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ambapo pia Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philipo Mpango ametunukiwa Tuzo hiyo aliyokqbidhiwa Mhe. Mchengerwa kwa niaba yake.
Post A Comment: