Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akiwa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ameshuhudia utiaji saini mkataba mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi 145 billioni utakaotekelezwa kwa miezi thelathini na mbili na kampuni ya Kichina.
Akimwakilisha Waziri wa Maji Jumaa Aweso,Mahundi amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa katika miji 28 nchini ukiwemo Songea utakaopandisha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 83 hadi asilimia 95.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameelekeza fedha nyingi katika Wizara ya maji akiwa na dhamira thabiti ya kumtua mama ndoo kichwani.
Katika hatua nyingine Mahundi amesema Wizara imenunua mitambo mitano ya utafiti wa maji na magari ishirini na tano kwa ajili ya kuchimba visima.
Amesema Wizara pia imejielekeza kuchimba mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji yanayotokana na mvua ili maji hayo yakivunwa yasaidie kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji.
Mahundi ametumia fursa hiyo pia kumpongeza Mbunge wa Songea Dkt Damas Ndumbalo kwa ufuatiliaji ili kuona wananchi wake wanapata maji safi na salama.
Aidha Mahundi amewataka vijana kujitokeza kufanya kazi katika mradi huo ili kujiongezea kipato.
Mahundi kwa kushirikiana na Waziri wa Maji na watendaji wote nchini watahakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati.
Post A Comment: