Naibu Waziri wa Maji amesema dhamira ya Wizara ya Maji na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani.
Ameyasema hayo wakati wa ukaguzi wa mradi wa maji uliofanywa na Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira Mkoani Tabora mradi wa Ziwa Victoria Ziba-Nkinga Wilaya ya Igunga utakaonufaisha Kata nne zenye Vijiji tisa unaogharimu shilingi 5.3bn kutoka mfuko wa Benki ya Dunia .
Kupitia mradi huo watu 29,780 watanufaika kama taarifa iliyotolewa na Mhandisi Hatari Kapufi Meneja RUWASA Mkoa wa Tabora inavyoeleza.
Mahundi amesema mradi umefikia asilimia 85 ambao unatarajiwa kukamilika machi 31,2023 ambapo ungekuwa na vituo viwili lakini baada ya pesa kubaki vituo vitatu zaidi vya kuchotea maji vitaongezeka na kufanya jumla ya vituo kuwa vitano.
Aidha Mahundi ameagiza wataalamu kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati na hawana visingizio kwa kuwa pesa zipo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira Jackson Kiswaga mbali ya kupongeza Serikali na Wizara kwa utekelezaji wa miradi ameshauri wasimamizi wa miradi wawe wataalam watakaosaidia makusanyo na ukarabati miradi inapoharibika ili iwe endelevu na Serikali ifikie malengo yake.
Mradi wa maji wa Ziwa Victoria ndiyo suluhisho pekee la kero ya maji kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo haina vyanzo vya maji vya uhakika.
Post A Comment: