Na John Mapepele
Wizara ya Maliasili na Utalii, imemuunga mkono Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipongeza Yanga katika ushindi wake wa leo dhidi ya TP Mazembe katika Kombe la Shirikisho.
Katika mechi ya leo iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamini timu ya Yanga imeweza kujinyakulia pointi zote tatu baada ya kuibamiza TP Mazembe mabao matatu kwa moja.
Kutokana na kupata magoli matatu, Yanga imejinyakulia milioni 15 kutoka kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alizoahidi ikiwa ni shilingi milioni 5 kila goli baada ya kumalizika kwa mchezo usiku huu ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa shilingi milioni 2.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa amefafanua kuwa Wizara yake itaendelea kutumia Michezo kuendeleza Utalii duniani.
" Na sisi Wizara ya Maliasili na Utalii tutatumia michezo kama hii kutangaza vivutio vya nchi yetu katika mabara yote, tunataka kuwajaza watalii hapa nchini ili wachangie kwenye uchumi wetu" amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Wizara nyingine zilizotoa fedha ni Ardhi, Fedha na Utamaduni Sanaa na Michezo ambazo pia kila moja imetoa milioni 2.
Ushindi huo unaifanya Yanga kushika nafasi ya tatu katika kundi D la mashindano hayo.
Katika mchezo huo Viongozi mbalimbali wa Serikali wamehudhuria wakiwemo Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe, Pindi Chana Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbasi na Katibu Mkuu wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu.
Post A Comment: