Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu wake Dkt. Hassan Abbasi leo, siku moja tu baada ya Waziri kuapishwa, wameanza kazi mara moja mjini Morogoro.
Katika hafla ya kukabidhi magari 22 ya doria kwa Taasisi ya Wanyamapori (Tawa), viongozi hao wameweka malengo makubwa katika kuigeuza wizara hiyo kiutendaji.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Abbasi amewaeleza watendaji wa Wizara hiyo kutarajia kazi kubwa itakayofanyika katika uhifadhi na kutangaza utalii.
“Katika wakati wetu watu watarajie kazi kubwa sana katika kuhifadhi lakini baada ya hapo tunawalinda simba ili iweje? Wizara hii inahitaji sana “promo” kubwa ili watalii waje hapa,” alisema.
Naye Mhe Mchengerwa alisema katika wizara hiyo kama watu walikuwa wanatembea sasa waanze kukimbia.
“Rais katoka kafanya filamu ya Royal Tour katuanzishia hili sisi leo tunafanyaje kutangaza utalii zaidi?? Katika wakati wetu mjiandae kwa kazi kubwa sana ya mchana na usiku ya kuitangaza nchi,” alisema Waziri Mchengerwa.
Aidha, Waziri pia amesisitiza watendaji wa Wizara hiyo kuwa wabunifu na kuachana na visingizio vya kukwamisha kazi na kusema katika wakati wake hakuna kuwaza kukwama.
Hafla hiyo imefanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) zilizopo mkoani Morogoro.
Post A Comment: