Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 15,2023 katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Februari 2023. Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 15,2023 katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Februari 2023.


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji amewahimiza Wafanyabiashara nchini kuendelea kuzingatia misingi ya ushindani wa haki katika kufanya biashara ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza uchumi kwa manufaa ya Wananchi wote.

Wito huo ameutoa leo Februari 15,2023 katika Ofisi za Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Februari 2023.

Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwenye kiasi cha mavuno ya mazao muhimu ya chakula kama mchele, mahindi, maharage na viazi mviringo, mahitaji ya bidhaa hizo kwenye nchi jirani yamekuwa makubwa kuliko uzalishaji hivyo, kuchangia kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula nchini na nchi jirani.

Aidha amesema Mfumuko wa bei nchini Tanzania ni wa kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na nchi jirani ambapo kwa Tanzania kiwango cha mfumuko wa bei ni asilimia 4.9 kwa mwezi Januari 2023 ikilinganishwa na asilimia 9.1 ya Kiwango cha mfumuko wa bei nchini Kenya , asilimia 10.4 nchini Uganda na asilimia 21.7 nchini Rwanda kwa mwezi Januari, 2023.

Dkt.Kijaji amesema Wizara inaendelea kuratibu ukusanyaji wa takwimu za bei za mazao na bidhaa muhimu kama vile vyakula na vifaa vya ujenzi kutoka kwenye masoko yaliyopo katika Mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia Wakusanya Taarifa za Masoko (Market Monitors) na Maafisa Biashara wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Takwimu hizi husaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika ukokotoaji wa kiwango cha mfumuko wa bei kila mwezi na kuweza kufanya tathmini ya upatikanaji wa mazao na bidhaa mbalimbali nchini". Amesema

Hata hivyo amesema mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula kama mahindi kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 750 na 1,750 kwa kilo. Bei ya chini haijaonyesha mabadiliko wakati bei ya juu imepanda ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari, 2023 ambayo ilikuwa kati ya Shilingi 750 na 1600 kwa kilo, na bei ya bidhaa ya Unga wa mahindi kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 1,500 na 2,100 kwa kilo. Bei ya unga wa mahindi haijabadilika ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023. Bei ya chini ipo katika Mikoa ya Geita na Manyara na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Kigoma na Mara.

Pamoja na haayo amesema Serikali inaendelea kufuatilia na kufanya tathmini ya bei za bidhaa muhimu ili kulinda maslahi ya wadau wote ikiwa ni pamoja na wazalishaji, wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa husika.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: