Na WMJJWM, DSM


Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amekutana na kuzungumza na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Kyle Nunas, katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es salaam Februari 23, 2023.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubaliana kushirikiana utekelezaji wa Programu mbalimbali hususan ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kufikia Kizazi chenye Usawa (EFG) eneo ambalo Tanzania ni Kinara.

Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kwamba, uimarishaji wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ni hatua muhimu kuelekea kuwafanya Wanawake waweze kufikika na kupeana uzoefu ambao utasaidia kwenye kusimama kiuchumi  jambo ambalo litachangia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kupitia mpango huo.

Hata hivyo, amesisitiza wadau wote kuongeza uwezeshaji wa Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii ili kuwezesha kuchochea mwamko wa jamii na mabadiliko ya fikra kuelekea kizazi chenye usawa kwenye maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake Balozi Kyle amesema Canada ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa kuanzisha afua mbalimbali zitakazisaidia kutoa elimu ya Afya na uzazi pamoja na uimarishaji wa Madawati ya Jinsia.

Katika kikao hicho Balozi wa Canada ameambatana na Mkuu wa Mashirikiano Bi. Helen Fytche pamoja na Mchambuzi Mwandamizi wa mipango kutoka ubalozi huo Bi. Taslim Madhani.

Share To:

Post A Comment: