Na WMJJWM, Kilimanjaro
Maafisa Maendeleo ya Jamii wametakiwa kuimarisha ufuatiliaji wa mafanikio na changamoto za upatikanaji wa mikopo ya wanawake kupitia 10% ya fedha za makusanyo ya Halmashauri na kuzipatia majibu kwa wakati kwa kushirikiana na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kwa mujibu wa mwongozo mpya wa mwaka 2022.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa agizo hilo kufuatia maoni ya Wanawake na Wafanyabiashara wa Masoko ya Mbuyuni na Manyema, Wilaya ya Moshi, mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake kiuchumi na fursa za mikopo ya Halmashauri ziara aliyofanya Februari 18, 2023.
Katika ziara hiyo Waziri Dkt. Gwajima kupitia maoni ya Wanawake hao amebaini changamoto ya wengi wao kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu mikopo hiyo na fursa za kuwawezesha kiuchumi. Hivyo, Dkt. Gwajima akalazimika kuweka bayana kuwa mpango wa uwezeshaji wanawake kiuchumi ni suala la kijamii ni vema jamii ifahamu kikamilifu mwongozo wa huduma hiyo na vikundi viainishwe na vifahamike kwa viongozi wa majukwaa hayo kwa ajili ya kuhamasishana wao kwa wao.
Amesisitiza kuwa, ushirikishaji wa taarifa utasaidia pia kuepusha vikundi vingine kuchukua fedha na kubadilisha matumizi kinyume na utaratibu, hivyo kushindwa kurejesha mkopo na kuathiri mpango huo.
Akitoa taarifa ya hali ya mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Afisa Maendeleo ya Manispaa hiyo Bi. Rose Minja amesema zaidi ya vikundi 423 kati vikundi 800 vimefaidika na mkopo wa sh. Bil. 2.4 kuanzia mwaka 2018.
Kwa upande wao baadhi ya wanawake wakieleza hali ya fursa wanazopata kupitia Halmashauri hiyo wamebainisha kwamba wengi wao hawapati taarifa za mikopo hiyo kama wanavyopata taarifa za mikopo mingine ya Taasisi za fedha binafsi.
"Tuliomba mkopo kuanzia mwezi wa sita Mwaka jana, nashangaa taratibu zote tumefanya lakini tukienda Manispaa hatupati taarifa yoyote na hatujui nini kinaendelea" amesema Mary Shayo kiongozi wa Kikundi cha Kinesi wa soko la Mbuyuni. "Wanawake wengi wamekuwa wakihitaji mikopo katika soko hili lakini inachelewa sana na hatujui tatizo liko wapi, wanaanzisha vikundi hadi wanakata tamaa" amesema Mustapha Waziri Soko la Manyema.
Katika ziara hiyo, Dkt. Gwajima amefanya mikutano na wananchi katika Kata tano (5) za Mabondeni Soko la Mbuyuni, Soko la Manyema, Kata ya Mji Mpya na Majengo za Manispaa ya Moshi na Kata ya Mabogini iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na ziara hizo zinaendelea nchi nzima.
Post A Comment: