Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumzia uchangiaji wa damu uliofanywa na watumishi wa ofisi yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma wakati akihitimisha shughuli za kijamii zilizofanywa na ofisi yake jijini Dodoma kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na jamii.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwaongoza watumishi wa ofisi yake kupata vipimo vya awali kabla ya kuchangia damu katika Kituo Kidogo cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwahamasisha watumishi wa ofisi yake kuchangia damu katika Kituo Kidogo cha Damu Salama katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini ACP. Ibrahim Mahumi na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Idara ya Mikataba ya Utendaji kazi Serikalini Bi. Zainabu Kutengezah.
Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakichangia damu katika Kitengo cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji wa damu.
Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakijiorodhesha kushiriki kuchangia damu katika Kituo Kidogo cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kujenga mahusiano na jamii.
Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. George Mkira akitoa shukrani kwa Uongozi na watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji.
********************************
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 13 Februari, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama, amesema watumishi wa ofisi yake wameunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kulinda rasilimaliwatu nchini kwa kuchangia damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma itakayowasaidia wananchi, watumishi wa sekta ya umma na binafsi wenye uhitaji.
Mhe. Jenista amesema hayo wakati akihitimisha shughuli za kijamii zilizofanywa na ofisi yake katika jiji la Dodoma kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na jamii.
Mhe. Jenista amesema, watumishi wa ofisi yake wamechangia damu ili kuiwezesha benki ya damu kuwa na akiba ya kutosha itakayokidhi mahitaji kwani anaamini damu hiyo licha ya kuilenga jamii lakini pia itawasaidia watumishi wa umma na wa sekta binafsi watakaopata changamoto ya uhitaji wa damu.
“Uchangiaji huu wa damu uliofanywa na watumishi wa ofisi yangu utaimarisha afya ya wananchi, watumishi wa umma na watumishi wa sekta binafsi ili wawe na tija katika kuleta maendeleo na ustawi wa taifa,” Mhe. Jenista amefafanua.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema damu iliyochangiwa na watumishi wa ofisi yake itawasaidia watanzania wote wenye uhitaji wa damu.
Kutokana uhitaji wa damu katika hospitali nyingi nchini, Mhe. Ndejembi ametoa wito kwa watumishi wa taasisi nyingine za umma kujitokeza na kuchangia damu katika benki ya damu ili damu hiyo itumike kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji.
“Uchangiaji huu wa damu ni mfano mzuri wa kuigwa na watumishi wa taasisi nyingine za umma kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anataka watumishi wa umma kuwa karibu na jamii na kuendelea kujenga mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mmoja wa watumishi waliochangia damu, Bi. Mariam Mwanilwa ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mishahara, Masilahi na Marupurupu amesema kuwa, anayo furaha baada ya kuchangia damu ambayo anaamini itaokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. George Mkira ameushukuru uongozi na watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa uamuzi wa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji wa damu.
Dkt. Mkira amesema, chupa 50 za damu zilizopatikana si haba kwani kwa makadirio damu hiyo itawahudumia watoto wenye uhitaji wasiopungua mia na hamsini.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetumia siku mbili kushiriki huduma za kijamii kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na wananchi.
Post A Comment: