Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa Uhifadhi na kutembelea vivutio vya Utalii nchini.
Ameyasema hayo leo alipofanya kikao na watendaji hao katika Chuo cha Wanyamapori cha Pasiansi jijini Mwanza.
Amesema ni vyema jamii ikaelimishwa juu ya uhifadhi kuanzia ngazi ya Vijiji, Kata, Wilaya na Mikoa ili wote wawe na uelewa wa pamoja ili kuwa na uhifadhi wenye tija na pia kurahisisha usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa .
Kwa upande wa masuala ya utalii Mhe. Masanja amesema kuwa kikao hicho kimekubaliana kuanza kutangaza utalii kwa kutumia fursa ya kushiriki kwenye matamasha mbalimbali kwa lengo la kuwajulisha wananchi umuhimu wa kutalii.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuwa wazalendo kwa kutembelea vivutio mbalimbali vilivyoko nchini.
“Nawaomba watanzania wote wawe wazalendo wakatembelee vivutio vya utalii kwani gharama ni ndogo sana haizidi fedha ya kitanzania shilingi elfu kumi (10).
Ametaja faida za kutalii ni pamoja na kujifunza, kupumzisha akili kwa kutoa msongo wa mawazo na pia kuvijua na kuvitambua aina mbalimbali za vivutio vilivyoko nchini.
Kikao hicho kimehudhuriwa na taasisi za Wizara zilizoko Kanda ya Ziwa ambazo ni Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Pasiansi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha Utalii Kampasi ya Mwanza na Idara ya Utalii.
Post A Comment: