Wanawake wa Tanga Mjini leo wamefanya Kongamano la kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanga Mjini na Tanzania kwa ujumla.

Kongamano hilo limefanyika leo ukumbi wa Regal Naivera Jijini Tanga ambapo Mgeni Rasmi ni Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu ambae pia ni Mbunge wa Tanga Mjini.

Kongamano hilo limeandaliwa na Jukwaa la Wanawake wajasiliamali wilaya ya Tanga chini ya Mwenyekiti wa Jukwaa Ndugu Aziza Ramadhan. Kongamano hilo la kumpongeza Rais Samia pia limelenga kuwajengea uwezo wa kiuchumi wanawake wa Tanga ili kuweza kuchangamkia fursa za maendeleo.

Mhe Ummy aliungana na wakina mama wa Tanga kumpongeza Mhe Rais Dr. Samia kwa kuendelea kutoa fedha za Elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpk kidato cha sita, ujenzi wa shule za msingi na sekondari, ujenzi wa vituo vya afya na Zahanati lakini kubwa ni kuendelea kuleta fedha kwa ajili ya upanuzi na uchimbaji kina katika bandari ya Tanga.

Mhe Ummy ameeleza kuwa kati ya shilingi bilioni 429.1 zilizotumika kuboresha Bandari ya Tanga shilingi bilioni 256.8 zimetolewa na Serikali ya Awamu ya 6 ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mhe Ummy Mwalimu alipokea Tuzo ya Rais Samia na kuwashukuru wanawake wa Tanga kwa uamuzi wao wa kumtia moyo Rais. Amewaomba wanaTanga wamuombee Mungu amjalie afya njema, busara na hekima ili aendelee kuiongoza vyema nchi yetu.

Kongamano hilo limehudhuriwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wajasirimali wanawake mkoa wa Tanga ndg Fatuma Hatib, katibu tawala wilaya ya Tanga ndg. Dalimina, Waheshimiwa Madiwani na wawakilishi wa taasisi mbalimbali.



Share To:

Post A Comment: