KWA utamaduni wa maeneo mbalimbali nchini Tanzania, unapotokea msiba wanaume ndiyo huongoza mazishi kuanzia uchimbaji kaburi, hata ibada mbalimbali pale kaburini.
Hata kama wanawake wataenda makaburini, kwa baadhi ya imani ambazo zinaruhusu hawatahusika na uchimbaji kaburi, au uingiaji ndani kaburini kwenda kuzika iwe mtoto au mtu mzima, ingawa kwa baadhi ya maeneo machache watoto wachanga waliozaliwa na kufariki muda huohuo huwa wanawake wanazika.
Sasa iko hivi wanaume wanaoishi Kitongoji cha Namanyere, Kata ya Majimoto Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi wamesusia kufanya shughuli za mazishi ya watoto wanaofariki kwenye kitongoji hicho, kwa madai ya kukithiri kwa idadi ya vifo vya watoto, hivyo jukumu hilo la kuzika linafanywa na wanawake.
Hali hiyo sasa imezua sintofahamu, kwani haijawahi kutokea kwenye kitongoji hicho kwa shughuli za mazishi kufanywa na wanawake badala ya wanaume.
Akizungumza mkazi wa kitongoji hicho, John Madirisha, amesema wanaume wamesusia kufanya shughuli za mazishi kutokana kuongezeka idadi ya vifo vya watoto kuanzia umri wa kuzaliwa hadi miaka miwili.
Amesema idadi hiyo ya vifo imekuwa kubwa na kuanza kuwatia hofu juu ya vifo hivyo na kuamini vinatokana na nguvu ya giza.
‘’Sisi tumechoka kuzika kila siku watoto wanakufa na hao wanaowaua ni baadhi ya wanawake wa kitongoji hiki kwa kisingizio cha surua, wazike wenyewe,’’ amesema Madirisha.
Naye Michael Masanja mkazi wa kitongoji hicho, ameeleza kuwa idadi ya vifo imekuwa ni kubwa kwenye kitongoji hicho, kwani watoto wanaofariki kwa wiki ni kati ya wanne hadi watano.
Amedai kuwa hapo nyuma kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa surua, lakini hadi sasa bado vifo vimeendelea, hali inayofanya kutokubaliana na vifo hivyo, kwani wanaamini kuna ushirikina unaoendelea kufanywa na baadhi ya wanawake kwenye kitongoji hicho kwa kisingizio cha ugonjwa wa surua.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Namanyere, Teresia Wikula amekiri kuwa ni kweli wanaume wa kitongoji hicho wamesusia kufanya shughuli za mazishi na shughuli hizo kwa sasa zinafanywa na wanawake.
Amebainisha kuwa kwa wiki wamekuwa wakizika watoto wanne mpaka watoto watano, hali ambayo haijawahi kutokea katika kitongoji hicho.
Hata hivyo amesema vifo hivyo ni kutokana na ugonjwa wa surua na sio ushirikina kama wanavyodhani wanaume wa eneo hilo.
Amesema maofisa wa afya wamekuwa wakifika kitongojini hapo na kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kutoa chanjo, lakini mwitikio wa wananchi hao umekuwa mdogo.
Post A Comment: