Na;Elizabeth Paulo,Dodoma


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi za jamii Masha J. Mshomba ametoa rai kwa waajiri wote nchini kuzingatia sheria za kazi na ajira kwa kutekeleza jukumu la kuwasilisha michango ya watumishi wao kwa mujibu wa sheria itakayowezesha ulipaji wa mafao kufanyika kwa wakati.


Mshomba ametoa rai hiyo leo alipokutana na waandishi wa habari katika ofisi za habari maelezo jijini Dodoma kueleza utekelezaji wa majukumu ya mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).


Amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023, Mfuko umeendelea kuimarisha mifumo na usimamizi wa fedha ili kuepuka mianya ya upotevu wa fedha.


“Kuendelea kumudu garama za uendeshaji pamoja na kulipa mafao stahiki kwa wastaafu na wanufaika wengine, Kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi mfuko umekua ukipata hati safi (Unqualified reports) kutokana na kaguzi zilizofanywa na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, Hivyo fedha za wanachama zipo salama”.Alisema


Katika nusu ya mwaka wa fedha iliyoishia Desemba 2022, Mfuko ulilipa mafao ya shilingi bilioni 2.6 kwa watumishi 183 waliofutiwa ajira kwa kukosa vyeti halali baada ya Mh. Rais Dkt Samia Suluhu Hasan  kueleza watumishi hao kulipwa mafao ya michango waliyochangia katika kipindi cha ajira zao.


“Mfuko ulilipa mafao ya shilingi bilioni 350 kwa wanachama, Wastaafu na Wanufaika wengine wapatao 80,339 ambapo malipo hayo yanajumuisha bilioni 2.5.”Alieleza Mshomba


Aidha amesema katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita  thamani ya mfuko imekua kwa kiasi kikubwa na thamani kuongezeka na kufikia shilingi trilioni 6.6 mwezi Desemba 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 39 kutoka shilingi trilioni 4.7 iliyofikiwa mwezi machi 2021.


Kadhalika amesema michango ya wanachama kwa mwaka 2022/2023 inatarajiwa kufikia shilingi trilioni 1.6 ambayo ni ongezeko la asilimia 14 ikilinganishwa na michango ya shilingi trilioni 1.4 kwa mwaka 2021/2022.



 Ameongeza kuwa kwa upande wa Uwekezaji, NSSF wana fursa za nyumba za makazi salama kupitia mfuko huo mwananchi anaweza kumiliki nyumba ya ndoto yake kwa kulipa gharama ya nyumba kwa mkupuo mmoja au kulipa kidogo kidogo wakati wakiendelea kuishi katika nyumba husika na nyumba hizo zipo Dungu, Mtoni Kijichi na Toangoma mjini Dar es Salaam.


Kadhalika amesema serikali imetekeleza mikakakati mbalimbali ya kuvutia wawekezaji wakubwa ikiwa ni pamoja na kupitia maonesho ya filamu ya The Royal Tour. 


“Mikakati hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Nyanzaga Goldmine, Kiwanda cha mbolea Intracom, Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato, Mgodi wa Uchimbaji wa Madini ya Nikeli (Tembo) uliopo Ngara, Daraja la Kigongo-Busisi Mwanza, kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo, mradi wa umeme wa Rusumo  na mradi wa reli ya kisasa ya SGR inakamilika,”amesema. 


Amesema miradi hiyo pekee imechangia takribani wanachama wapya 33,066 na kwa ujumla mkakati huo wa Serikali umechangia katika ongezeko la wanachama na michango inayokusanywa na Mfuko. 


Sambamba na hayo amesema baada ya maboresho ya sekta ya Hifadhi ya jamii ya mwaka 2018 NSSF lilipewa jukumu la kuhudumia sekta binafsi na sekta isiyo rasmi kwakutambua asilimia kubwa ya watanzania wapo katika kundi la wanaojiajiri nakuwa sekta isiyo rasmi.


“Baada ya kupitishwa kwa sheria, NSSF  ilipeleka pendekezo la maboresho ya mafao katika mpango wa sekta isiyo rasmi, Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuusimamia sekta ya Hifadhi ya Jamii imeridhia maboresho hayo yenye lengo la kuwavutia watanzania wengi walio kwenye sekta isiyo rasmi kujiunga na kunufaika na mafao pamoja na huduma zitolewazo na NSSF”.Alisema na kuongeza


 “Matarajio ya kuzindua ni mwishoni mwa mwaka wa fedha 2022/2023 na nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi wenzangu katika sekta isiyo rasmi tuwe tayari kujiunga na kuchangia NSSF ili muweze kunufaika na huduma zitakazokuwa zinatolewa.”

Share To:

Post A Comment: