Na Imma Msumba ; Karatu

UTATA wa mabilioni ya fedha umeibuka katika ujenzi wa nyumba za wakuu wa Idara Halmashauri ya  wilaya ya Karatu, Arusha ambapo nyumba hizo hazijakamilika kwa mwaka wa pili sasa pamoja na fedha kutumika.

Katika ujenzi wa nyumba hizo serikali kuu ilitoa kiasi cha shilingi Milioni 150 ambazo zilitarajiwa kumaliza ujenzi wa nyumba hizo za wakuu wa Idara katika mfumo tatu katika sehemu moja.

Mfumo huo wa nyumba tatu sehemu moja ulitumika wakati serikali kuu ilipotoa Milioni 90 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kama hizo katika  Hospitali ya wilaya na hadi sasa ujenzi wake umekamilika na nyumba zipo tayari kwa matumizi.

Baada ya ujenzi wa nyumba kusuasua kwa kipindi cha muda mrefu Halmashauri ilitoa milioni 40 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa awamu ya kwanza ili kukamilisha ujenzi huo lakini haukukamilika ambapo kwa awamu ya pili Halmashauri imetoa tena kiasi cha Milioni 39 ili kumalizia ujenzi wa nyumba hizo lakinii mpaka sasa nyumba hizo hazijakamilika na zitahitaji fedha nyingine kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo.  Mpaka sasa zimeshatumika zaidi ya milioni 229.

Pamoja na wingi wa fedha hizo ambazo serikali kuu ilitoa na Halmashauri, bado ujenzi wa nyumba haujakamilika hali ambayo imepelekea taharuki kwa wananchi wa Karatu ambao fedha zao za mapato ya ndani ndizo zinazotumika kwa sasa kukamilisha ujenzi huo.

Akizungumza nasi moja ya Madiwani wa Halmashari hiyo ya Karatu ameeleza “Kitu cha ajabu ni kwamba wameendelea kuomba pesa, tuliongeza milioni 39 haijatosha tukaongeza milioni 40 tena nikiwa na madiwani wenzangu wanafahamu katika nyakati zote tulikataa kuongeza pesa ambayo ni halali ya wananchi wa Karatu”

“Hatua hazijawahi kuchukuliwa kwa wale waliobadilisha ramani ya ile nyumba tunaingizia hasara Halmashauri na huu ni  uzembe maana ramani ilikuja kutoka serikali kuu wahandisi wakasema wanaiboresha mpaka leo walioingizia Halmashauri hasara zaidi ya Milioni 80 hawajachukuliwa hatua yoyote wapo na nyumba haijakamilika mpaka sasa" Aliongezea

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu Dr. John Lucian Mahu amekiri kupokea kwa fedha kutoka Serikali Kuu shilingi millioni 150 huku akisema kama Halmashauri ya wilaya wamepata hasara kubwa ya kuongeza fedha katika umaliziaji wa Nyumba hizo.

Kadhalika amesema kabla ya mwezi Machi 2023 familia mbili za Wakuu wa Idara wanatarajiwa kuhamia huku Halmashauri ikitarajia kutoa fedha kiasi cha shilingi millioni 23 kwaajili ya kumalizia nyumba ya Tatu ya Wakuu hao.

“Tuliunda kamati ya Uchunguzi na kwa Uchunguzi huo fedha zimetumika vizuri tatizo ni aliyekua Mkurugenzi  kipindi hicho aliongeza ramani ya Ujenzi wa nyumba hizo kwa kuongeza vyumba katika kila nyumba hii imetuumiza kwasababu tumeanza kutumia fedha zetu za mapato ya ndani katika kukamilisha hilo jengo wakati tulikua tutekeleze miradi mengine.”Alisema

“kwa mujibu wa wahandisi wetu bado kiasi cha shilingi millioni 23 zakutumika kumalizia ujenzi wa nyumba ya Tatu na sisi kama Halmashauri tumeshaweka kwenye bajeti.”


Share To:

Post A Comment: