Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala (aliyevaa suti) akisaini mkataba wa ukarabati wa kivuko cha MV. MAGOGONI pamoja na mkandarasi African Marine and General Engineering Company Ltd. inayotoka Mombasa nchini Kenya huku akishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo, Mhe. Mussa Azan Zungu (Mb), Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika leo eneo la Magogoni Kigamboni jijini Dar es Salaam. Gharama ya kukarabati kivuko hicho ni shilingi bilioni 7.5.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala kulia pamoja na mkandarasi kutoka kampuni ya African Marine and General Engineering Company Ltd. inayotoka Mombasa nchini Kenya wakionyesha mikataba yao waliyosaini leo mbele ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa ya ukarabati wa kivuko cha MV. MAGOGONI ambao unagharimu shilingi bilioni 7.5.

PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA)

*****************************

Na. Alfred S. Mgweno (TEMESA)

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) leo imesaini mkataba wa ukarabati wa kivuko cha MV. MAGOGONI wenye thamani ya shilingi Bilioni 7.5. Mkataba huo umesainiwa leo katika eneo la kivuko cha Magogoni Kigamboni jijini Dar es Salaam kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro N. Kilahala na mkandarasi African Marine and General Engineering Company Ltd. inayotoka Mombasa nchini Kenya na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo, Mhe. Mussa Azan Zungu (Mb), Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge, Wakuu wa Wilaya pamoja na viongozi mbalimbali wa Taasisi nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema ukarabati wa Kivuko cha MV. MAGOGONI ni juhudi na mikakati ya Serikali katika kuboresha miundombinu mbalimbali ya usafirishaji nchini na kuongeza kuwa ukarabati huo utakapokamilika utaharakisha na kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi waishio katika Wilaya ya Kigamboni, Ilala na maeneo mengine

’’Madhumuni ya ukarabati wa kivuko hiki ni kuhakikisha huduma inayotolewa na kivuko hiki ni salama kwa watumiaji na hivyo kuwaondolea wananchi kero ya usafiri inayotokana na kuchakaa kwa kivuko hiki. Kivuko hiki kilijengwa mwaka 2008 na kina uwezo wa kubeba Tani 500 yaani abiria 2000 na magari madogo 60 na ni kiunganishi muhimu kati ya maeneo ya Wilaya ya Kigamboni na Wilaya ya Ilala.’’ Amesema Profesa Mbarawa na kuongeza kuwa wakati umefika sasa wa kivuko hicho kufanyiwa ukarabati mkubwa.

’’Wakati kivuko hiki kinafanyiwa ukarabati kutakuwa na changamoto ya usafiri, kwahiyo niwaombe sana wakazi wa Dar es Dalaam hasa maeneo haya watumie kwa wingi Daraja la Nyerere ili kupunguza msongamano katika kivuko hiki, amesema Profesa Mbarawa na kuongeza kuwa wakati wa kutoa tenda Serikali inaangalia mambo mawili makubwa, ’’Jambo la kwanza tunaangalia bei, nani ni mwenye gharama za chini, kama alivosema Mtendaji Mkuu TEMESA, mkandarasi ambaye alikuwa na bei ya chini ilikuwa ni bilioni 7.5, aliyemfuatia wa pili alikuwa na bilioni 10, tofauti ya bilioni 2.5, kama hii ni pesa yako wewe utampatia nani mkataba wa kazi hiyo? Nawaachieni mjibu,’’ alimaliza Profesa Mbarawa.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azan Zungu akizungumza katika hafla hiyo amewaomba wananchi wa maeneo hayo kuvumilia changamoto ya kukosekana kwa kivuko hicho wakati kitakapokuwa kwenye matengenezo kwa kuwa matengenezo hayo yanalenga kuleta huduma bora na kivuko hicho kuwa salama kwa ajili ya kutumiwa na wananchi hao.

Naye Mbunge wa Kigamboni Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika hafla hiyo ametoa rai kwa Serikali kutoa fursa kwa sekta binafsi kuruhusiwa kuanza kutoa huduma ya kivuko katika eneo hilo.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro N. Kilahala akisoma taarifa fupi ya mradi huo amesema mkandarasi African Marine and General Engineering Company Ltd. Ataanza rasmi ukarabati wa kivuko hicho mara baadaa ya kulipwa malipo ya awali na anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi sita.

’’Kivuko cha MV. MAGOGONI ni Tegemeo kubwa kwa wananchi wa Kigamboni kutokana na uwezo wake wa kubebea abiria na magari mengi kwa wakati mmoja hivyo ukarabati huu utawezesha kivuko hiki kutoa huduma ya uhakika na tija kwa wana Kigamboni.’’ Amesema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa kazi ya ukarabati wa kivuko hicho itahusisha kazi za chuma, kuondoa mabati yaliyochakaa ya muundo wa chini na wa juu, ujenzi wa milango mipya ya kushushia na kupakia abiria, ukarabati wa chumba cha kuongozea kivuko, ufungaji wa injini mpya nne aina ya Caterpillar pamoja na gia boksi zake, matengenezo makubwa ya pampu jeti, marekebisho makubwa ya mfumo mzima wa umeme na elektroniki wa kivuko, kufungwa kangavuke (majenereta) mapya mawili, matengenezo ya mfumo wa tahadhari ya moto, kufunga kamera za CCTV, kuweka vifaa vya kisasa vya kuongozea kivuko, vifaa vya tahadhari na vya uokozi, pamoja na kupaka rangi kivuko chote.


Mtendaji Mkuu alimaliza kwa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kukubali kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo na miradi mingine na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya Serikali na wananchi kwa ujumla.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: